ATCL: Ndege ya Tanzania imetua nchini baada ya kuachiliwa huru Afrika kusini:

Ndege ya Air Tanzania imetua nyumbani Tanzania mwendo wa saa mbili unusu usiku huu baada ya kuachiliwa huru na mahakama ya Afrika Kusini.

Shirika la ndege hiyo imeandika katika ukurasa wake wa Tweeter kuwa safari za ndege hiyo kuelekea Afrika kusini zitarejea siku ya ijumaa.

Mapema leo Mahakama Kuu ya jimbo la Gauteng imeamuru ndege ya Air Tanzania iliyokuwa ikishikiliwa nchini Afrika Kusini kuachiwa mara moja.

Mwandishi wetu wa Afrika Kusini anasema kuwa utaratibu wa kuiachia ndege hiyo kurejea Dar es Salaam kutoka uwanja wa ndege wa OR Tambo jijini Johannesburg unaendelea.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Dkt Damas Ndumbaro aliyekuwepo mahakamani ameileza Newsday Swahili kuwa Tanzania imeridhishwa na uamuzi wa mahakama.

Mkulima ambaye alipeleka shauri hilo mahakamani Hermanus Steyn na kupata kibali cha kushikiliwa ndege hiyo, hakuridhishwa na hukumu ya awali na kukata rufaa.

Mwandishi wa Newsday Swahili anaripoti kuwa Bw Steyn amedondoshwa pia kwenye rufaa yake na kutupiliwa mbali na mahakama.

Dkt Ndumbaro ambaye pia ni wakili amesema kama Steyn bado ana madai yeyote, inafaa arudi kwenye mahakama za Tanzania na kusikilizwa.

"Oh, niamini, raisi (John Magufuli) tayari ameshapewa taarifa (ya hukumu)," mwandishi wa Newsday Swahili aliyepo mahakamani anamnukuu Dkt Ndumbaro akisema.

Ndumbaro pia amesisitiza kwa kuwa serikali ya Tanzania imeshamlipa Steyn dola milioni 20, maana yake wapo tayari kumalizia bakaa ya deni, lakini mkulima huyo "anatakiwa kurudi katika mahakama za Tanzania, na aache kuihusisha Afrika Kusini."

Baada ya ya kushindwa kwa kesi ya awali na hatimaye rufaa, wakili wa Steyn ameiambia Newsday Swahili kuwa uamuzi wa mahakama: "Ni kushindwa moja kwa moja kwa haki, na mteja wangu anaona kuwa ameonewa. Bw. Steyn amepoteza kikomboleo cha mali na hii inamaanisha kuwa hawezi kukata rufaa bila ya ndege kuwa imezuiliwa."

Jaji aliyesikiliza rufaa amesisitiza kuwa Afrika Kusini haina mamlaka ya kisheria (jurisdiction) ya kuliamulia jambo hilo.

Kwa nini ndege ilizuiliwa?

Ndege hiyo aina ya Airbus A220-300 ilikuwa imeshikiliwa katika uwanja wa Oliver Tambo jijini Johannesburg kwa amri ya mahakama.

Hermanus Steyn alifungua kesi ya fidia dhidi ya serikali ya Tanzania.

Steyn alikuwa anamiliki ardhi, mifugo na mali nyingi ambazo zilitaifishwa na serikali ya Tanzania miaka ya 1980.

Ilipofika miaka ya 1990 walikubaliana fidia atakayolipwa, kwa ujumla wake dola milioni 33 na tayari ameshalipwa dola milioni 20 kati ya hizo.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Tanzania, kwa mujibu wa mkulima huyo imeacha kulipa deni hilo, na hatua ya kuomba ndege kushikiliwa ilikuwa moja ya harakati zake za kutaka kumaliziwa deni.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?