Maandamano Kenya: 'Msiwaue, wapigeni risasi mguuni' Ruto awaambia polisi

Rais wa Kenya William Ruto ameapa kutumia ''mbinu zozote zinazohitajika'' kuhakikisha amani na utulivu inadumishwa nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa makazi ya polisi jijini Nairobi Rais Ruto aliyeonekana kuwa na hasira alisema yuko tayari kufanya lolote kukomesha wimbi la maandamano ya machafuko la hivi majuzi ambalo limesababisha vifo vya zaidi ya watu 40. "Inatosha, hatuwezi kuruhusu hili liendelee, tutatumia njia zozote kuleta utulivu nchini," alisema.
Kenya imeshuhudia wimbi la maandamano dhidi ya serikali, ambayo yalianza Juni 2024 kupinga nyongeza ya kodi. Maandamano hayo, hasa yakiongozwa na vijana, wanaofahamika 'Gen-z' hata hivyo yamebadilika na kujumuisha wito wa kumtaka Rais Ruto ajiuzulu, kukomesha ukatili wa polisi na utawala mbaya.
Katika hotuba yake ya kwanza kwa umma kuhusu suala hilo, tangu duru ya hivi punde zaidi ya maandamano mapema wiki hii alisema, ''Ni viongozi wanaowafadhili vijana kutekeleza vitendo hivyo, na tunawafuatilia!," akiwaonya wale anaodai wanafanya njama ya kumng'oa kwenye wadhifa wake wa urais akisema kuwa wanaotaka kuwania nafasi yake 'wakutane naye 2027' - kwenye uchaguzi ujao wa urais ulioratibiwa.
''Nchi hii haitaharibiwa na watu wachache wanaotaka kufanya mabadiliko ya serikali kwa kutumia njia zisizo za kikatiba, hilo halitakubaliwa.''
End of Iliyosomwa zaidi
Pia aliapa kuwachukulia hatua kali waandamanaji wanaodaiwa kuteketeza vituo mbalimbali vya polisi wakati wa maandamano ya hivi majuzi.
"Yeyote anayechoma biashara na mali ya watu, basi apigwe risasi mguuni, aende hospitalini akielekea mahakamani. Naam, wasiue, bali wapige risasi na kuvunja miguu. Kuharibu mali za watu si sawa," alisema.
Alisema mashambulizi dhidi ya maafisa wa polisi na majengo kama vile vituo vya polisi, kama yale yaliyoshuhudiwa wakati wa kumbukumbu ya maandamano ya kupinga mswaha wa Fedha wa Juni 25-2024, yatachukuliwa kama ugaidi.
"Wale wanaoshambulia polisi wetu na vituo vya polisi, wanatangaza vita. Ni ugaidi, na tutakabiliana nao kikamilifu. Hatuwezi kuwa na taifa linaloongozwa na ugaidi na kutawaliwa na ghasia; hilo halitafanyika chini ya uangalizi wangu," Ruto alisema.
Kenya imeshuhudia ongezeko la maandamano ya kupinga serikali katika miezi ya hivi huku waandamanaji wakilalamikia utawala wa Ruto kwa kuchangia kupanda kwa gharama ya maisha na msururu wa dhuluma dhidi ya wakosoaji wa serikali.
Maandamano hayo yamesababisha vifo, majerahu na utekaji nyara.
Wakosoaji wanalaani polisi kwa ukatili na matumizi ya risasi za moto dhidi ya waandamanaji wasio na silaha wakati wa maandamano yanayoongozwa na vijana.




Maoni
Chapisha Maoni