Kwanini Somaliland ina matumaini na ujio wa Trump?
Watu wengi huko Somaliland wanaamini kwamba Marekani, chini ya rais ajaye Donald Trump, itakuwa nchi ya kwanza duniani kuitambua jamhuri hiyo iliyojitangazia uhuru wake.
Eneo hilo lilijitangazia uhuru miaka 33 iliyopita baada ya Somalia kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
"Donald ni mwokozi wetu. Ni mtu mwenye hekima. Mungu ibariki Marekani," anasema mwanafunzi wa chuo kikuu Aisha Ismail.
Anazungumza nami kutoka Hargeisa, mji mkuu wa Somaliland - jiji lililo umbali wa kilomita 850 (maili 530) kaskazini mwa Mogadishu, Somalia.
Kwa wale walio Mogadishu, Somaliland ni sehemu ya Somalia.
"Nina shaka kwamba Donald Trump anaijua Somaliland ni nini, au iko wapi," anasema Abdi Mohamud, mchambuzi huko Mogadishu.
Kwanini wana matumaini?
Warepublican wenye ushawishi wanashinikiza jambo hilo hilo, akiwemo Mbunge Scott Perry ambaye mwezi uliopita aliwasilisha mswada unaopendekeza Marekani kuitambua rasmi Somaliland.
Ni baada ya kuchapishwa mpango wa Project 2025, mwezi April 2023, mpango wa muhula wa pili wa Trump, ambao ulichapishwa na Wakfu mashuhuri wa mrengo wa kulia wa Heritage Foundation na zaidi ya mashirika 100 ya kihafidhina.
Waraka huo unataja maeneo mawili pekee ya Afrika katika sehemu ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara - Somaliland na Djibouti - na inapendekeza "kutambuliwa kwa serikali ya Somaliland kama mbadala wa Marekani kwa Djibouti."
Msanifu mkuu wa fikra za Republican Afrika, hasa linapokuja suala la Somalia, ni Joshua Meservey, kutoka Wakfu ya Hudson Institute.
"Kesi ya Somaliland kwa Marekani inavutia sana," anasema. "Nadhani suala la kutambuliwa bila shaka litajadiliwa."
Maafisa wakuu wa wanaoshughulikia masuala ya Afrika chini ya Trump, akiwemo aliyekuwa Katibu Msaidizi wa Mambo ya Nje wa Masuala ya Afrika, Tibor Nagy, na mjumbe wa Afrika, Peter Pham, wanaunga mkono uhuru wa Somaliland.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somaliland, Abdirahman Dahir Adan anasema, "ikiwa Marekani inataka kambi ya kijeshi hapa tutawapa."
Lakini hakuna hakikisho kwamba utawala unaokuja utafuata mwongozo huo. Jambo moja liko wazi, Marekani tayari imeanza kubadili msimamo wake kuhusu Somaliland.
Somalia imeigharimu Marekani katika masuala ya kifedha na rasilimali tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakati miili ya wanajeshi 18 wa Marekani ilipokokotwa katika mitaa ya Mogadishu baada ya helikopta za Marekani kudunguliwa na wapiganaji wa koo za Somalia.
Mapigano hayo yanayojulikana kama "Black Hawk Down," yalikuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea kwa Marekani tangu Vita vya Vietnam.
Somalia inasemaje?
"Hatua yoyote ya kutambua uhuru wa Somaliland sio tu itakiuka mamlaka ya Somalia lakini pia itavuruga eneo hilo," anasema Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Ali Mohamed Omar.
Umoja wa Afrika na mataifa mengine yenye nguvu duniani yanaamini kuwa kuheshimu mipaka ya eneo hilo ni muhimu.
Kuitambua Somaliland kunaweza kuanzisha msururu wa watu wanaotaka kujitenga kote ulimwenguni kudai kutambuliwa kwa maeneo wanayodai.
Pia inaweza kusababisha jeshi la Marekani kuondoka Somalia. Chini ya urais wa Joe Biden takriban wanajeshi 500 wa Marekani wamewekwa nchini Somalia - wakifanya operesheni maalum na kutoa mafunzo kwa kikosi cha Somalia.
Marekani ina kambi ya anga huko Baledogle, kaskazini-magharibi mwa Mogadishu, na hufanya mashambulizi ya anga ya mara kwa mara dhidi ya waasi wa Kiislamu.
"Kujiondoa kutaleta ombwe kubwa la usalama, kuamsha vikundi vya kigaidi na kutishia usalama sio tu wa Somalia bali pia pembe pana ya Afrika," anasema Omar.
Eneo muhimu
Ukanda wa pwani wa Somalilanda unapita kwenye mojawapo ya njia za meli zenye shughuli nyingi zaidi duniani.
Waasi wa Houthi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran wamechukua nafasi ya maharamia wa Somalia kama wasumbufu wakuu katika eneo hilo na mashambulizi yanasalia kuwa tishio kubwa kwa biashara ya kimataifa na kulisogeza eneo hilo karibu na vita vya Mashariki ya Kati.
Wingi wa kambi za kijeshi kwenye pwani ya Pembe ya Afrika unaitia wasiwasi Marekani, ambayo ilianzisha kituo chake kikubwa zaidi cha kijeshi huko Djibouti mwaka 2002.
Urusi inaitazama Port Sudan. Djibouti ina vikosi vingi vya kigeni vikiwemo vikosi vya China, ambao sio tu wana kituo cha kijeshi lakini pia wanaendesha bandari kubwa.
Kambi kubwa zaidi ya Uturuki kwenye ardhi ya kigeni iko kando ya mwambao wa Somalia kusini mwa Mogadishu.
Marekani imeishutumu China kwa kuingilia shughuli zake nchini Djibouti kwa kupiga mwanga kwenye macho ya marubani wake wa kikosi cha anga na wana nia ya kuhamia kwingine.
Pia inataka kuvuruga Mpango wa China wa ujenzi wa miundombinu (Belt and Road Initiative,) ambao utachukua sehemu kubwa ya Afrika.
Bandari ya Berbera, iwe unaiona kama sehemu ya Somaliland au Somalia, ina mengi ya kutoa kama njia mbadala.
Wakati wa utawala wa Biden, maafisa wakuu wa Marekani, akiwemo mkuu wa Kamandi ya Marekani ya Afrika (Africom), walitembelea eneo la Berbera, lenye njia ya kurukia ndege ya kilomita 4 iliyojengwa na Umoja wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi.
Hili baadaye lilitambuliwa na Marekani kama eneo la dharura la kutua kwa vyombo vya anga - na mshirika wa Trump, Elon Musk anavutiwa na eneo hilo.
Mwaka 2022, Sheria ya Kitaifa ya Ulinzi ya Marekani ilirekebishwa na kuijumuisha Somaliland, ili kuimarisha ushirikiano na uwezekano wa kuunda uhusiano thabiti wa kidiplomasia na kiuchumi.
Mwanadiplomasia wa Somaliland mwenye makazi yake nchini Marekani anasema, kwa Warepublican wanaotaka itambuliwe Somaliland: "itagemea jinsi watakavyomueleza Trump. Inabidi waifanye ivutie; inabidi wamshawishi."
Tayari kuna mazungumzo huko Somaliland kwamba eneo hilo litatumika kama "mahali pa kupokea" wahamiaji wasio na vibali watakaorudishwa kutoka Marekani na utawala wa Trump, na utawala huo utalitambua eneo hilo.
Msomi wa Marekani Ken Menkhaus, ambaye amefuatilia masuala ya Somalia kwa miongo kadhaa, anasema.
"Kuna uwezekano mkubwa tutaona mabadiliko makubwa katika sera ya Marekani kuelekea Somaliland na Somalia."
Maoni
Chapisha Maoni