Air Tanzania: Kesi ya utaifishwaji ya mwaka 1980 yazua mgogoro upya:

Mahakama kuu ya nchini Afrika Kusini imeizuia ndege ya Air Tanzania kuruka nchini humo kutokana na kesi ya zamani ambayo haina uhusiano wowote na masuala ya ndege kati ya nchi Afrika kusini na Tanzania.

Msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania amefafanua kuwa ndege hiyo imeshikiliwa kutokana na kesi ya fidia inayomhusu raia wa Afrika Kusini Bwana Hermanus Steyn na Serikali ya Tanzania.

Mtu huyo ambaye alikuwa anamiliki ardhi, mifugo na mali nyingi, zilitaifishwa na serikali ya Tanzania miaka ya 1980 na walifikia makubaliana na serikali ya Tanzania.

"Kesi hii ni madai ya muda mrefu ya fidia ya ardhi iliyotwaliwa tangu miaka ya 1980 huko hivyo sio kesi kwamba ni ATCL ndiyo inadaiwa, Hapana.Tunaipambania ndege hii kwa maslahi ya Taifa letu na tunaamini siku moja itarudi kuendelea na shughuli zake za kawaida" msemaji wa serikali Dkt. Hassan Abbasi.

Msemaji huyo ameeleza kuwa ndege zote sita za Tanzania ziko salama isipokuwa ndege moja ambayo imezuiliwa nchini Afrika Kusini.

Aidha Dkt. Abbas amesema kuwa serikali ya Tanzania ina kesi na raia wa Afrika wa kusini ambaye alifikia makubaliana na serikali hiyo na fidia alilipwa kwa kiasi kikubwa na kimebaki kiasi kidogo.

Hivyo aliamua kwenda kwenye mahakama ya serikali ya Afrika kusini kutekeleza hukumu ya kesi ya nchi nyingine na utaratibu upo kisheria.

Hukumu tayari imesomwa na hata upande wa Tanzania una haki wa kupinga ameeleza msemaji huyo.

"Kesi ya msingi bado haijatekelezwa, ya kuwa Tanzania itakubali kulipa madai yake au la.

Yeye alichagua mahakama kumsikiliza bila serikali ya Tanzania kuwepo ndio maana wao walikuwa hawana taarifa," Dkt.Abbas alifafanua.

Hata hivyo msemaji huyo wa Tanzania amesema kuwa mawakili wako kazini na hawezi kuhakikishia kuwa itarudi lini lakini anaamini kuwa ndege hiyo itarudi.

Mpaka sasa Mamlaka nchini Afrika Kusini haijatoa tamko lolote kuhusiana na hatua hiyo.

Ndege hiyo ilikuwa inatoka Afrika Kusini kwenda jijini Dar es Salaam.

Lakini Kwa mujibu wa balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ndege hiyo imezuiliwa kwa amri ya Mahakama Kuu ya mjini Johannesburg.

Ripoti ya baadhi za vyombo vya habari nchini Tanzania zinaashiria kuwa abiria waliokuwa ndani ya ndege ya Air Tanzania iliyozuiliwa kuondoka katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo mjini Johannesburg wametafutiwa usafiri mbadala katika nmashirika mengine ya ndege.

Gazeti la Mwananchi linaripoti kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Ladislaus Matindi amesema ''Kuna safari nyingi zitakazoathiriwa kutokana na kushikiliwa kwa ndege hiyo aina ya Air Bus A220-300''

Bwa. Matindi ameliambia Mwananchi kuwa abiria waliokata tiketi wataarifiwa iwapo kutakuwa na mabadiliko yoyote ama ipo kama ilivyopangwa.

Tayari Shirika hilo limetoa taarifa rasmi kupitia mtandao wake wa Twitter kuwaomba radhi wateja wake na kuongeza kwamba kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake itafanyia marekebisho safari zake.

Msemaji wa Mkuu wa serikali ya Tanzania ameiambia Newsday Swahili kuwa wanasheria wa nchi hiyo wamewasili nchini Afrika Kusini kufuatilia suala hilo na kwamba wakikamilisha mchakato huo watatoa taarifa kamili.

Taarifa iliyotolewa Ijumaa usiku na katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dk Leonard Chamuriho ilieleza kuwa serikali kupitia ofisi ya mwanasheria mkuu inafuatilia suala hilo.

Baadhi ya raia nchini Tanzania wamekuwa wakijadili nini huenda imeeifanya mahakama ya Afrika Kusini kuzuia ndege hiyo.

@majanimabichi ameandika katika Twitter yake akiuliza: Kwa nini mahakama ikamate/izuie ndege? Kuna jambo limejificha nyuma ya pazia. Toeni sababu.

@PaternusP aliandika:Tulitazame kwa umakini na kidiplomasia. Kutikiswa lazima watatutikisa kutupima REACTIONS zetu. Hakuna haja ya kupaniki juu ya jambo hili. Adapt, Improvise, Overcome.

@catfish88854732 aliandika South Africa ; mahakama ziko huru .Rais wa Sauzi kamwe hawezi kuingilia mahakama.

Wengine walichukua jukumu la kuwafafanulia wenzao maana ya hatua hiyo

Shirika la ndege la Tanzania linalomilikiwa na serikali lilizindua safari yake ya kwanza kwenda mjini Johannesbur, Afrika Kusini mwezi Juni mwaka huu katika hatua ambayo lengo lake lilitajwa kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini ulifikiwa mwaka 2002 baada ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini kununua hisa za Shirika la Ndege la Tanzania.

Lakini ushirikiano huo ulimalizika baada ya serikali ya Tanzania kununua hisa za Shirika la Ndege la Afrika Kusini ili kumiliki Shirika hilo kwa 100%.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Global Travel Industry, miaka miwili baadae Shirika la ndege la Afrika Kusini liliwasilisha kesi mahakamani mjini Dar es Salaam katika jaribio la kutaka kulipwa deni lake la dola milioni 4.1 lililokuwa likiidai ATCL.

Juhudi za serikali za kuliongezea mtaji Shirika hilo muda mfupi baada ya kuajitennga na SAA bado hazijaleta tija baada ya ATCL kushindwa kupata faida kama ilivyo ahidi.

Kutokana na matukio ya kibiashara yaliopia Mamlaka ya Air Tanzania ilionywa na Bunge kuwa makini zaidi katika ushirikiano wake wa kibiashara na Shirika la Ndege la China , likisema mpago huo unastahili kuwafaidi wafanyikazi wake na Watanzania wote kwa jumla.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?