Rais John Magufuli ampongeza Albert Chalamila kwa kuwatandika viboko wanafunzi wa Chunya.

Rais John Magufuli amempongeza mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kwa kuwachapa viboko wanafunzi wa kidato cha tano na sita wa Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya kwa madai ya kuhusika kuchoma moto mabweni mawili ya shule hiyo.

''Leo nilikuwa naongea na mkuu wa mkoa wa Mbeya nikamwambia nakupongeza sana kwa kuwatandika wale viboko na nikawaambia uliwatandika viboko vichachee...haiwezekani serikali tunatoa mabilioni kwa ajili ya kujenga madarasa na shule halafu mtoto anaenda kuichoma''. Alisema rais Magufuli.

Rais huyo ambae yupo ziarani katika eneo la nyanda za juu kusini amesema kuwa alimwambia Bwana Chalamila awafukuze watoto wote waliohusika na tukio hilo .

''Nikamwambia watoto hao wote fukuza wote, kwa hiyo watoto wote wamefukuzwa, na bodi imevunjwa kwasababu ile pia uzembe wa bodi ya shule hiyo..eti haki za binadamu, haki za binadamu watoto wawe na viburi vya kipumbavu hivyo. Ni lazima tuache mchezo katika maendeleo'', alisema.

Ameonya kuwa kurudi shuleni kwa watoto hao ni lazima baba zao walipie gharama za majengo yaliyoharibiwa na akaagiza kuwa wale ambao walihusika wapelekwe jela.

Rais huyo wa Tanzania ameeleza kuwa mabadiliko ya sheria kuhusu viboko ndio chanzo cha vurugu mashuleni kama zile zinazodaiwa kutekelezwa na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kiwanja

''Nafikiri kama mahali tulikosea ile sheria ikafanyiwa marekebisho wawe wanatandikwa viboko... Ati mkuu wa mkoa alitandikwa viboko hata Ulaya wanatandika viboko...Kiboko kinafundisha''

Amewasihi wazazi wawatandike viboko watoto wao nyumbani ili kujenga taifa lenye watoto wenye nidhamu.

Video ya Mkuu wa mkoa Albert Chalamila akiwachapa viboko wanafunzi hao wa shule ya bweni ya Kiwanja kwa madai ya kuchoma moto mabweni mawili ilienea kwenye mitandao ya kijamii

Tayari watoto hao wamefukuzwa shuleni na kupigwa faini. Hata hivyo awali Bwana Chalamila alikosolewa kwa kuwapiga wanafunzi na waziri wa serikali za mitaa Suleman Jafo, ambaye alisema kuwa hakuna sheria inayomruhusu Mkuu wa mkoa kuwaadhibu wanafunzi.

Mkuu huyo wa mkoa alitetea kitendo chake cha kuwatandika wanafunzi hao akisema kuwa yeye ni mkuu wa mwalimu mkuu na kwa hivyo ana wajibu wa kile kinachofanyika katika shule hiyo.

Video hizo zilionyesha kikundi cha wanafunzi wakiwa wamelala chini huku nyuso zao zikitazama ardhini wakati Bwana Chalamila akiwatandika viboko vitatu vitatu kila mmoja, huku wanafunzi wengine wakitazama.

Adhabu ya viboko haizuiwi kisheria nchini Tanzaniana hutumiwa kwa kawaida kuwapa nidhamu wanafunzi.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?