Mbwana Samatta ailiza Anderlecht ya Vincent Kompany

Mabingwa wa ligi ya Ubelgiji Genk waliilaza timu inayoongozwa na mchezaji wa zamani wa Manchester City Vincent Kompany - Anderlecht 1-0 katika siku ya tano ya ligi hiyo ya Jupiler Pro.

Baada ya timu hizo mbili kukabiliana , Genk hatimaye ilikuwa kifua mbele katika dakika ya 55.

Kiungo wa kati wa klabu hiyo Junya Ito alimpatia pasi murua mshambuliaji wa Genk raia wa Tanzania Mbwana Samatta ambaye hakupoteza wakati na kucheka na wavu.

Anderlecht ilijaribu kutafuta bao la kusawazisha , lakini walipata pigo baada ya mchezaji wao Phillip Sandler kuondolewa kunako dakika ya 68 kabla ya nahodha Vincent Kompany pia naye kupandishwa katika machela kunako dakika ya 74 na jeraha.

Siku ya Alhamisi, Kompany aliwachilia kazi yake ya ukufunzi wakati wa siku za mechi ili kucheza na badala yake ameamua kuchukua unahodha wa timu hiyo.

Klabu hiyo ya Ubelgiji imechukua pointi mbili pekee kati ya 15 katika mechi zake tano za kwanza na hivyobasi kuongeza msururu wao mbaya katika miaka 21.

Miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Andelecht alikuwa mchezaji mwenza wa Kompany Samir Nasri.

Jeraha hilo la Kompany huenda likamzuia kutoshiriki katika mechi yake ya kumuaga Etihad katika kipindi cha wiki tatu zijazo.

Kompany ambaye alijiunga na Andelecht kama mkufunzi mchezaji alitibiwa kandokando ya uwanja kabla ya kufungwa donge la barafu katika mguu wake wa kulia.

Anatarajiwa kurudi Manchester tarehe 11 September ili kusherehekea huduma yake ya miaka 11 akiichezea klabu hiyo ya Etihad.

Huo ni ushindi wa pili mfululizo wa Genk huku naye Mbwana Samatta akijikita miongoni mwa wachezaji wanaoongoza kwa magoli katika ligi hiyo kufuatia hatrick yake katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Waasland Beveren.

Miezi iliopita mchezaji huyo alizivutia klabu za Uingereza kama vile Aston Villa Watford, Leicester na Burnley baada ya kuonyesha hamu yake ya kutaka kujiunga na klabu za ligi ya Uingereza.
Klabu ya Brighton imekuwa ikimfuatilia Samatta kwa muda mrefu na kocha wa timu hiyo kwa msimu uliopita Chris Hughton alikuwa akivutiwa sana na mchezaji huyo.

Samatta alijiunga na Genk akitokea TP Mazembe Januari 2016 ambapo alitia saini mkataba wa kumuweka katika klabu hiyo hadi msimu wa 2019/20.

Msimu uliopita, 2018/19 bila ya shaka ulikuwa bora kabisa kwake toka alipojiunga na klabu hiyo.

Alifunga magoli 23 ya ligi na magoli 9 kwenye michuano ya ligi ya Europa. Pia amepata tuzo ya Ebony ambayo hutuzwa mchezaji bora mwenye asili ya Afrika nchini Ubelgiji.

Pia ametoa mchango mkubwa kwa klabu hiyo kuchukua ubingwa wa ligi baada ya kuukosa kwa miaka minane.

Samatta alianza Maisha yake ya soka akiwa kinda na klabu ya Mbagala Market kisha akasajiliwa na Simba zote za Dar es Salaam Tanzania.

Mazembe walimsajili 2011 akitokea Simba.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?