Hisia kali baada ya watu 8 kukamatwa kufuatia ajali ya gari la mafuta Kagera Tanzania

Kuna msemo wa kiswahili usemao "Binadamu ameumbwa kusahau" na kiuhalisia jambo hilo halipingiki hata kidogo.

Na swali kubwa ni Je, huwa tunajifunza kutokana na makosa?

Ni siku chache tu zimepita ambapo Tanzania ilipata janga kubwa la ajali ya moto huko mkoani Morogoro mara baada ya lori la mafuta kuanguka na kuuwa watu zaidi ya 100 na huku majeruhi wengine wakiendelea kupata tiba mpaka hii leo.

Chanzo cha vifo hivyo kilitokana na watu kusogelea gari lililoanguka na kuchota mafuta.

Na hapo jana ajali nyingine imetokea mkoani Kagera, ambapo lori la mafuta lilianguka wilayani Ngara wakati likiwa linatokea Rwanda kuelekea Dar es salaam na cha kushangaza watu walikimbilia tena kuchota mafuta bila uoga wowote.

Kufuatia ajali hiyo ambayo imesababisha kifo cha dereva wa lori, jeshi la Polisi mkoani Kagera limewashikilia watu 8 kwa tuhuma za wizi wa mafuta na kukamata lita 300 za mafuta kutoka mikononi mwa wanakijiji katika wilaya ya Ngara.

 Ni vyema tukajiepusha na matukio yoyote yale yanayoweza kutuletea madhara, watu wote waliochota mafuta au kujaribu kuchota mafuta katika lori hilo wanapaswa kukamatwa na kutiwa kwenye vyombo vya sheria," Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti alitoa agizo la watu hao kukamatwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Revocatus Malimi alisema "Nilidhani kwamba ajali ya Morogoro ilikuwa fundisho lakini hali ni tofauti na bora tuliwahi kufika kuwafukuza".

Tabia ya watu kukimbilia maeneo ambayo hatari ilikemewa vikali na wataalamu wa Idara ya zimamoto nchini Tanzania wakati ajali ya Morogoro ilipotokea, lakini tahadhari hiyo haijafahamika kama ilieleweka.

Kamishna wa operesheni Jeshi la zimamoto na uokoaji, Bwana Billy J. Mwakatage alitoa angalizo alipohojiwa na BBC hivi karibuni : ''Gari lolote likianguka ikiwa na shehena ya mafuta haipaswi kukaribiwa, mtu yeyote asiye mtaalamu hapaswi kusogelea, na si mafuta tu ni bidhaa nyingine zinazosafirishwa na vyombo vya usafirishaji kama sumu pamoja na kemikali hatari''.

Kamishna amesema sasa hivi sasa kuna mfumo wa utoaji elimu kuhusu namna ya kupambana na majanga ya moto, elimu inayotolewa kwenye shule mbalimbali.

''Idara ya zimamoto imepita kwenye sule za msingi na sekondari tukiwafundisha. Tumeanzisha fire clubs zinazofundisha namna ya kuchukua tahadhari wakati wa majanga ya moto ili waelewe madhara ya moto pia tahadhari za kuchukua''.

''Na tumeanza kwa shule kwa watoto wadogo, kujua namba ya dharura, si tu kwa majanga ya moto, bali pia uokozi na mengine yote isipokuwa jinai kuwafundisha kuifahamu namba ya dharura ya jeshi la zimamoto na uokoaji, 114''. Alieleza kamishna.

Lakini pamoja na elimu hiyo kutolewa shuleni, bado kuna watoto na vijana katika video inayosambaa kwenye mtandao ikionyesha namna wanavyochota mafuta katika lori lililoanguka huko Kagera.

Gari la mafuta lalipuka tena Uganda na kuua

Baadhi ya matukio ya mikasa ya malori ya mafuta Afrika

January 31 2009 Kenya: Moto uliwachoma watu waliokuwa wakifyonza mafuta wakati lori la mafuta lilipoanguka huko Molo kaskazini mwa mji wa Nairobi na kuwaoa watu 122.

Julai 2, 2010, DR Congo: Takriban watu 292 waliuawa wakati lori la mafuta lilipolipuka mashariki mwa kijiji cha Sange. Baadhi ya waathiriwa walikuwa wakijaribu kuiba mafuta baada ya ajali hiyo huku wengine wakitazama mechi ya kombe la dunia.

Oktoba 6, 2018 DR Congo: Takriban watu 53 waliuawa baada ya lori la mafuta kugongana na gari jingine na kushika moto katika barabara kuu ya mji mkuu wa Kinshasa

Septemba 16 2015 Sudan Kusini: Watu 203 walifariki na wengine 150 kujeruhiwa wakati watu walipokuwa wakijaribu kuiba mafuta.

Novemba 17 2016 Msumbiji: Takriban watu 93 waliuawa wakati lori la mafuta lililokuwa likibeba petroli lilipolipuka magharibi mwa taifa hilo . Mamia walikuwa wakijaribu kufyonza mafuta kutoka katika gari hilo.

Julai 12 2012, Nigeria: Takriban watu 104 walifariki walipokuwa wakijaribu kuchukua mafuta kutoka kwa lori la mafuta baada ya kuanguka kusini mwa jimbo la River State.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?