Eric Kabendera: Mwandishi wa Tanzania kuendelea kuzuiliwa baada ya mahakama kuahirisha kesi dhidi yake

Mwandishi wa habari za uchunguzi , Erick Kabendera ataendelea kuzuiliwa jela baada ya Kesi ya uhujumu Uchumi inayomkabili ikuahirishwa hadi Septemba 12 mwaka huu.

Hii ni baada ya upande wa Serikali kudai kuwa upelelezi wa Kesi hiyo bado haujakamilika.Wakili wake Jebra Kambole ameiambia Mahakama ya hakimu Mkaazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa waleta mashtaka wanapaswa kuhimizwa wakamilishe upelelezi kwa Wakati na kuiomba Mahakama isisitize juu ya Hilo

Wakili Kambole pia amesema kuwa afya ya Kabendera ianendelea kuzorota baada ya kupata tatizo la upumuaji inapofika usiku tangu Agosti 21 hali iliyomfanya kushindwa kutembea kwa siku mbili.

Aidha ameiomba Mahakama hiyo iliamuru Jeshi la Magereza kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili mtuhumiwa ili aweze kupatiwa vipimo.

''Kwa kuwa mteja wetu hajapata huduma ya matibabu tunaomba Mahakama ielekeze maafisa wa magereza kumpeleka katika hospitali yoyote ya serikali akapimwe '' alisema wakili huyo.

Hata hivyo Wakili wa Serikali, Simon Wankyo ameipinga hoja hiyo kwa kudai kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina Mamlaka ya kutoa amri yoyote ile isipokuwa Mahakama kuu.Aidha Hakimu Rwizile ambaye anasikiliza Kesi hiyo amepata udhuru na kushindwa kufika mahakamani hapo.Kabendera ambaye ni Mwandishi wa kujitegemea aliyekuwa akichapisha habari zake katika vyombo mbalimbali nchini na ulimwenguni alikamatwa nyumbani kwake Mbweni, viungani mwa jiji la Dar es Salaam na watu wanaodhaniwa kuwa ni maafisa wa polisi mnamo Julai 29, 2019.

Kabendera alipandishwa kizimbani Agosti 5 na kusomewa mashtaka matatu ya ubadhirifu wa kiuchumi .

Katika mashtaka hayo Kabendera anatuhumiwa na kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini Tanzania, shtaka la pili ni la kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za kitanzania.

Kosa la tatu ni la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni mia moja na sabini.

Kwa mujibu wa mashtaka yaliowasilishwa, Kabendera anadaiwa kuyatekeleza hayo baina ya Januari 2015 na Julai mwaka huu mjini Dar Es Salaam na kwa baadhi ya makosa anadaiwa kuyafanya kwa ushirikiano wa watu ambao hawakuwepo mahakamani.

Makosa yote hayana dhamana na Kabendera anaendelea kusota rumande.

Kumekuwa na wasiwasi ndani na nje ya Tanzania kuhusu namna ambavyo amekamatwa, na taswira inayotokana na hatua hiyo kwa uhuru wa yombo vya habari nchini humo.

Pia baadhi ya wanaharakati wameonyesha kushangazwa na kubadilika kwa yaliominika kuwa ndio makosa anayotuhumiwa nayo.

Awali maafisa wa polisi na wale wa idara ya uhamiaji walisema anachunguzwa kuhusu utata wa uraia wake. Baadaye mawakili wake walitoa taarifa wakieleza mteja wao atashtakiwa kwa kuhusika na ripoti iliyochapiswha katika jarida la The Economist, lakini mahakamani kibao kikageuka tena na kuwa kesi ya ubadhirifu wa kiuchumi.

"Tunaisihi serikali ya Tanzania kutoa hakikisho la mchakato wa kutenda haki kisheria kwa raia wake, kama ilivyotambua kwamba ni haki ya msingi na kuridhia kwenye mikataba mbali mbali ya haki za kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa, miongoni mwao ikiwemo azimio la kimataifa la haki za kirai na kisiasa," inaeleza sehemu ya tamko la awali la Marekani na Uingereza juu ya wasiwasi huo.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?