Wajir Kenya: Watu sita wauawa na wapiganaji wa al-Shabab

Takriban watu sita wamefariki katika kaunti ya Wajir kaskazini mashariki mwa Kenya siku ya Ijumaa baada ya watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi al-Shabab kushambulia basi walilokuwa wakisafiri.

Walioshuhudia waliambia Newsday Swahili  kwamba wapiganaji kadhaa waliokuwa wamejihami walishambulia basi hilo lililokuwa likielekea Mandera na kuwalenga watu wasiotoka katika eneo hilo baada ya kuwatenga kutoka kwa abiria wengine.

Kisa hicho kinadaiwa kufanyika kati ya miji ya Wargadadud na Kutulo .

Kulingana na gazeti la Daily Nation nchini Kenya kamanda wa polisi katika kaunti hiyo Stephen Ngetich amethibitisha tukio hilo lakini hakuweza kutoa idadi kamili ya walioathiriwa.

Bwana Ngetich amesema kwamba kikosi cha maafisa maalum tayari kimetumwa katika eneo hilo.

''Naweza kuthibitisha kwamba kundi moja la watu waliojihami walishambulia basi ambalo lilikuwa linaelekea Mandera siku ya Ijumaa jioni ijapokuwa bado hatujapata habari kamili kuhusu idadi ya waliouawa'', alinukuliwa akizungumza na gazeti la Daily Nation.

Basi hilo la Madina linadaiwa kushambuliwa mwendo wa saa kumi na moja jioni.

Shambulio hilo linajiri mwezi mmoja baada ya wapiganaji wa al-Shabab kushambulia kituo cha polisi cha Wajir katika jaribio la kutaka kuwaachilia huru washukiwa wawili wa ugaidi ambao walikuwa wanazuiliwa katika kituo hicho.

Kundi la wapiganaji wa al- Shabab nchini Somalia ambalo limekuwa likitekeleza mashambulio hayo mara kwa mara katika eneo hilo limekiri kutekeleza shambulio hilo likisema kuwa limewaua takriban watu 10.

Katika taarifa iliochapishwa katika mojawapo wa tovuti zake , kundi hilo linasema limewalenga abiria wasiokuwa Waislamu katika basi hilo.

Kisa hiki kimetokea katika barabara ambayo takriban Wakenya 28 waliokuwa wakiabiri basi moja walishambuliwa na kuuawa miaka mitano iliopita.

Barabara hiyo ipo karibu na mpaka wa Somalia.

Tutazidi kukupasha zaidi ....



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?