Je juhudi za upatikanaji wa pedi zinazaa matunda A. Mashariki?

Serikali ya Rwanda imetangaza kuondoa ushuru wa nyongeza ya thamani (VAT) kwa taulo za hedhi katika hatua ya kusaidia wanawake na wasichana kupata vifaa hivyo kwa urahisi.

Mashirika ya kusaidia wanawake nchini humo yamekuwa yakipaaza sauti kutaka serikali kutoa taulo za hedhi hata kwa bure.

Hatua ya kuondoa ushuru wa nyongeza ya thamani kwa taulo zinazotumiwa na wanawake wakiwa katika hedhi imetangazwa na wizara ya maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia kwenye ukurasa wake wa Twitter
Wizara imesema kwamba ni uaamzi unaolenga kurahisishia akinamama kupata taulo hizo.

Lakini je hii ni suluhu ya tatizo?

Kwa kawaida maduka katika mji mkuu wa Rwanda Kigali na kwengineko nchini, bei ya paketi moja ya sodo(vitaambaa vya hedhi) huuzwa kati ya franga za Rwanda mia 900 na elfu moja, ambayo ni kama nusu ya dola 1, ukiondoa ushuru wa nyongeza ya thamani sokoni tofauti itakuwa ya franga chini ya 200.

Kwa mwananchi wa kipato cha chini, bei ya franga 700 bado ni ya juu: ''Kwa maoni yangu hatua hiyo haina maana hata kidogo. Unafikiri aliyekosa franga elfu 1 ya kununua taulo ya hedhi atapata mia franga 900? sidhani kwamba wanamsaidia msichana kwa lolote,Labda wangesema kwamba mtu akiwa na franga elfu 1 atapata taulo mbili hapo ingekuwa ni afadhali'', mkazi huyu wa Kigali aliiambia Newsday Swahili

Mashirika ya kutetea haki za wanawake na watu binafsi katika mataifa ya Afrika Mashariki wamekua wakipaza sauti kutaka taulo za hedhi zitolewe bure kama ilivyo katika baadhi ya sehemu kwa mipira ya kondomu.

'' Bado bei ya taulo ya hedhi iko juu kwa sababu inategemea idadi ya taulo ambazo mtu anahitaji akiwa katika hedhi. Kuna wanaohitaji zaidi ya moja.Nafikiri serikali ingezingatia namna ya kushusha bei ya taulo za hedhi. Kama vile watu wanafikiria kugawa mipira ya Kondomu kwa bure kwa nini hata taulo za hedhi zisitolewe kwa bure?'', anasema Mwanaharakati wa masuala ya wanawake nchini Rwanda Dusabe Aliane.

Upatikanaji wa taulo za hedhi si tatizo kwa wanyarwanda pekee.
Bi Janet Mbugua Ndichu anasema dunia inapaswa kuelekeza juhudi zake katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za hedhi ni wa kudumu na kuhakikisha zinapatikana kwa bei nafuu, na kuhakikisha uhifadhi wa zile zilizotumiwa na usafi kwa ujumla.

Nchini Kenya juhudi mbali mbali zimekuwa zikifanyika kujaribu kupaza sauti ili kuwasaidia wanawake hususan wasichana wa shule za sekondari kupata taulo za hedhi.

Bi Janet Mbugua Ndichu kutoka taasisi ya INUA DADA ambayo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wasichana katika shule za sekondari nchini Kenya wanapata sodo anasema ameipongeza hatua iliyopigwa na Rwanda na kuongeza kuwa :'' Kikanda , Kenya inaongoza katika kuendeleza sera ambazo zinaendelea inapokuja katika udhibiti wa usafi wa hedhi. Kenya pia iliondoa kodi ya ongezeko la thamani VAT. Lakini athari za hatua hizi bado watumiaji hawajazihisi''

''Malengo yanapaswa kuwa katika kuhakikisha taulo za hedhi zinaweza kununuliwa na watumiaji. Kwa sasa bado wengi hawawezi kuzinunua kutokana na bei yake'', anasema Bi Janet Mbugua Ndichu.

Anasema licha ya juhudi zake za kusaidia upatikanaji wa vitambaa vya hedhi kwa wasichana, jamii nzima inapaswa kuwa na jukumu la kuhakikisha bidhaa na taarifa juu ya hedhi zinapatikana. ''Dunia inapaswa kuelekeza juhudi zake katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za hedhi ni wa kudumu na kuhakikisha zinapatikana kwa bei nafuu, na kuhakikisha uhifadhi wa zile zilizotumiwa na usafi kwa ujumla vinajumuishwa'' , anasema

Hata hivyo bado baadhi ya wasichana wanakosa kuhudhulia masomo yao kutokana na ima kutopatikana au kukosa uwezo wa kifedha wa kuzinunua bidhaa hiyo muhimu.

Mapema mwezi Septemba aibu ya kukosa pedi ilimfanya mwanafunzi mmoja nchini Kenya ajiue baada ya kudaiwa kuzomewa darasani kwa kuwa sare yake ya shule ilichafuka na madoa ya damu alipokuwa kwenye hedhi.

Mama wa Mwanafunzi huyo mwenye miaka 14 alisema binti yake alijinyonga baada ya kudhalilishwa na mwalimu wake, vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti.

Je Tanzania hali ikoje?

Licha ya Serikali na wadau wa maendeleo kufungua milango zaidi kwa watoto wa kike kupata elimu bado Nchini Tanzania wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa taulo za kike (pedi) kujisitiri wakiwa katika siku zao hasa katika maeneo ya vijijini.

Changamotohiyo inawakumba zaidi wasichana wanaoishi vijijini ambao hulazimika kukaa nyumbani mpaka siku zao ziishe, wakati huo huo wakipitwa na vipindi vya masomo darasani jambo linaloathiri mwenendo wa ufaulu.

Katika baadhi ya maduka Jijini Dar es Salaam taulo za hedhi (pedi) zinakadiriwa kupatikana kwa bei ya Sh1,300 hadi Sh 2,000 za Tanzania kwa pakiti yenye pedi nne na wakati mwingine bei hiyo hutofautiana kutoka eneo moja hadi lingine.

Wanaharakati wanaotetea haki za wanawake wamekuwa wakitoa wito taulo hizo zifikishwe na kutolewa bure kwa wanawake hususan wa maeneo ya vijijini.

Baadhi hutumia mbinu mbadala kuzuwia hedhi.

Tatizo la ukosefu wa vitambaa vya hedhi limekuwa ni jambo la aibu miongoni mwa wasichana wengi barani Afrika na hata baadhi yao kuamua kutumia mbinu mbadala kuepuka aibu ya hedhi.

Mfano katika taifa la Namibia Nchini Namibia, si kwamba hedhi ni jambo la aibu tu bali hata wengi miongoni mwa wasichana ni maskini sana wasiokuwa na uwezo wa kununua taulo za hedhi.

Baadhi ya wasichana hupewa tembe za kuzuwia ujauzito kama njia ya kuepukana na aibu ya hedhi: Aibu ya hedhi hatari kwa wasichana

Katika baadhi ya shule nchini Rwanda imeanza kampeni ya kuweka chumba maalumu kwa watoto wa kike kujisetiri ikiwa wamekuwa hedhi bila kutarajia,ambapo wanapata mahitaji yote kwa bure.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?