Victoire Ingebire: Kiongozi wa chama cha upinzani FDU Inkingi nchini Rwanda atangaza kuanzisha chama kingine cha upinzani

Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda, Bi. Victoire Ingabire amejiuzulu kuwa mkuu wa chama cha FDU na kuanzisha chama kipya cha kisiasa, chama cha maendeleo na uhuru kwa wote-''DALFA-UMURINZI''(Development And Liberty For All).

Ingabire ameeleza sababu zilizompelekea kuchukua hatua hiyo ni kutokana na chama cha FDU kuwa nje ya Rwanda hivyo kinakuwa hakihusiani na hali halisi nchini Rwanda.

Katika mazungumzo na waandishi wa habari mjini Kigali, Bi. Victoire Ingabire ameeleza pia kuwa amechoka kuendelea kuongoza chama kwenye mtandao kwa sababu wafuasi wake wengi na wakuu wengine wa chama hicho wako nje ya nchi na kwamba wakati umewadia kuwa na chama kinachobainisha matatizo kikiwa ndani ya nchi.

Ingabire ameondoa wasiwasi wa kwamba amekisaliti FDU kwa manufaa ya chama tawala RPF.

''Kuna waliosema kwamba ninakwenda kuwa mpambe wa chama tawala RPF, sio kweli.

Ni vizuri watu wafahamu kwamba siasa lazima ipige hatua.

Haingewezekana kuendelea kuongoza chama kupitia mtandao. Nilizungumza na wafuasi wakuu wa FDU tukakubaliana kwamba heri kuwepo chama cha watu walioko ndani ya nchi kuliko kuwa na chama kilicho na uongozi nje ya nchi'' Ingabire ameeleza.

FDU Inkingi kinasemaje?

Chama cha FDU Inkingi katika taarifa rasmi, kimetoa shukran kwa kujitolea kwa mwenyekiti huyo wa zamani Ingabire na kumtakia kila la kheri katika uzinduzi wa chama chake kipya Dalfa.

Kadhalika kimeeleza kwamba Justin Bahunga ndiye aliyeteuliwa kwa sasa kuwa kaimu mwenyekiti wa chama hicho,wakati kkukisubiriwa kikao cha chama kuchukua hatua za kulijaza pengo hilo.

Ingabire alikuwa miongoni mwa waasisi wa chama cha FDU na kukiongoza kwa miaka 13, hata alipokuwa gerezanialiendelea kuitwa kiongozi wa chama hicho.

Baadhi wanaona kwamba kuondoka kwake katika chama hicho ndio mwanzo wa kusambaratika, lakini yeye anasema haoni hivyo.

Mwandishi wa BBC mjini Kigali anaeleza kwamba kumekuwa na hisia katika siasa za Rwanda kwamba FDU kilikuwa kimeanza kuwa kama mzigo mzito kwake Ingabire.

''Tulipoanzisha FDU tulikuwa wengi. Kilichotokea ni kama vile mtoto anavyokuwa mtu mzima na kuacha kuishi kwa wazazi wake.

Siwezi kufurahia kusambaratika kwa FDU , jambo la pili si kwamba mimi ndiye nilikuwa ndani ya chama wala chama hakikuwa mimi'' ameeleza Ingabire.

Anasema atakiandikisha chama chake kipya na kuziheshimu sheria za nchi.

Baada ya Ingabire kutoka gerezani kwa msamaha wa Rais mwaka uliopita chama cha FDU kiliendelea kuhusishwa na kesi nyingi za ugaidi na makundi ya waasi dhidi ya Rwanda huku Ingabire akiripoti mara kwa mara polisi kuhojiwa kuhusu makundi ya waasi.

Victoire Ingabire Umuhoza alizaliwa oktoba tarehe tatu mwaka 1968.

Ni mke na mama wa watoto wa tatu.

Amesomea Sheria na masuala ya uhasibu na hatimaye kufuzu kwa shahada ya uchumi na biashara nchini Uholanzi.

Tangu mwaka 1997, Ingabire amejihusisha na harakati za upinzani nchini Rwanda akiwa mafichoni Uholanzi.

Aliteuliwa na muungano wa kundi la viongozi wa upinzani ambao una wanachama nchini Rwanda, barani Ulaya, Marekani na Canada.

Mnamo mwezi Januari mwaka 2010 Bi Ingabire alirejea Rwanda kutoka mafichoni nchini Uholanzi baada ya kutajwa kuhusika kwenye mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ili kugombea uchaguzi wa urais.

Mwezi Aprili mwaka 2010, aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani.

Alikamatwa baadaye na kufikishwa mahakamani ambapo yeye na washirika wake wanne, (Kanali Tharcisse Nditurende, Luteni kanali Noel Habiyaremye, Luteni Jean Marie Vianney Karuta na Meja Vital Uwumuremyi), walifunguliwa mashataka ya uhaini.

Alizuiliwa kugombea uraisi wa Rwanda kufuatia mashtaka yaliyokuwa yanamkabili.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?