Maandamano ya Iran: Umoja wa Mataifa umehofia watu kuuwawa.

Watu kadhaa huenda wakawa wamepoteza maisha nchini Iran tangu siku ya Ijumaa wakati wa maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama za mafuta ya petroli, Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binaadamu.

Msemaji wake amewataka maafisa usalama kutotumia nguvu kupita kiasi, ikiwemo kufyatua risasi, na ametaka mtandao wa intaneti urejeshwe.

Shirika la Amnesty International limesema limepokea ripoti za kuaminika kuwa waandamanaji 106 katika miji 21 wamepoteza maisha.

Haijulikani hali ikoje hivi sasa kwa sababu ya kufungiwa kwa huduma ya intaneti, kulikoanza Jumamosi jioni, lakini maandamano yameendelea kufanyika katika miji kadhaa mikubwa na midogo.

Maandamano yalizuka siku ya Ijumaa baada ya serikali kutangaza kupanda kwa gharama za petroli kwa 50% hadi kufikia riali 15,000 kwa lita moja sawa na kuwa madereva watapaswa kununua lita 60 kila mwezi kabla ya gharama kupanda kufikia riali 30,000.

Rais Hassan Rouhani amesema serikali inafanya hivyo kwa faida ya Umma na kuwa fedha zilizopatikana zinapelekwa kwa raia walio na uhitaji.

Hatahivyo, uamuzi ulifikiwa huku kukiwa na ghadhabu kubwa nchini humo ambapo uchumi tayari unayumba kutokana na vikwazo vya Marekani vilivyowekwa mwaka jana pale raisi Donald Trump alipoachana na mkataba wa nyukilia na Iran.

Vikwazo vimesababisha biashara ya usafirishaji wa mafuta kuanguka na thamani ya riali kuanguka, hali iliyofanya bei ya bidhaa kuongezeka.

Mpaka Jumapili, maandamano yalifikia miji 100, shirika la habari nchini nchini Iran, Fars lilisema.

Takribani benki 100 na maduka 57 yamechomwa, na takribani watu 1,000 wamekamatwa, liliongeza.

Ripoti zisizo rasmi kutoka kwa vyanzo mbalimbali zimesema takribani watu 200 wameuawa na wengine 3,000 wamejeruhiwa katika kipindi cha siku tano zilizopita.

Lakini mamlaka za Iran zimesema watu wachache wamepoteza maisha.

Vikosi vya usalama vilirekodiwa picha za video vikiwafyatulia risasi waandamanaji: familia za wale waliouawa zimesema mamlaka zimekataa kuwapa miili ya wapendwa wao kwa ajili ya maziko.

Kumekuwapo na askari wengi wa usalama katika viwanja mbalimbali vya wazi na kwenye mitaa ikubwa, wanafunzi wengi wa vyuo vikuu wamekamatwa na mahakama imeonya kuwa kutuma picha za video na kuzisambaza ni kosa la jinai.

Msemaji wa serikali amesema hali 'ilitulia' siku ya Jumatatu na imetabiri kuwa ''kesho na siku itakayofuata hatutakuwa na masuala yoyote kuhusu maandamano''.

Hata hivyo, video zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha maandamano yakiendelea katika maeneo mbalimbali usiku wa Jumatatu.

Maafisa watatu wa usalama pia waliuawa mjini Tehran, vyombo vya habari nchini humo vilieleza.

Siku ya Jumanne, msemaji wa ofisi ya kamishna wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za binaadamu aliuambia mkutano wa wanahabari mjini Geneva kuwa wanafahamu juu ya ripoti kuhusu ukiukwaji wa kanuni za kimataifa katika matumizi ya nguvu, ikiwemo kufyatua risasi, dhidi ya waandamanaji.

Rupert Colville amesema ni vigumu kuthibitisha kwa ujumla idadi ya vifo, lakini vyombo vya habari nchini Iran na baadhi ya vyanzo vingine vimesema watu kadhaa huenda wamepoteza maisha wakati wa maandamano katika majimbo karibu nane ya nchini humo.

''Tunazitaka mamlaka za Iran na vikosi vya usalama kuepuka kutumia nguvu nyingi kusambaratisha watu waliokutana kwa amani ''.

''Pia tunawataka waandamanaji kufanya maandamano kwa amani, bila kufanya vurugu au kuharibu mali,'' aliongeza.

Bwana Colville pia ametoa wito kwa serikali ya Iran kuheshimu haki ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani na kuitaka irejeshe huduma za intaneti .

Amesema Umoja wa Mataifa inatambua uwepo wa changamoto za kiuchumi zinazokabili Iran, kwa sehemu ikisababishwa na vikwazo vya Marekani.

Lakini ameonya kuwa kudhibiti kwa nguvu maandamano kwa maneno na silaha kunafanya mazingira kuwa mabaya zaidi.

Raisi Rouhani alisema siku ya Jumapili: ''Watu wana haki ya kuandamana, lakini maandamano ni tofauti na ghasia.

Hatupaswi kuruhusu matendo ya kutishia usalama katika jamii.''



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?