Mmoja afariki polisi wakituliza vurugu mkoani Mwanza

Mwanza. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema John Lulyeho (39) amefariki dunia baada ya kujeruhiwa kwa risasi wakati polisi wakituliza vurugu kwenye ranchi ya mifugo ya Mabuki iliyopo Wilaya ya Misungwi.

Akizungumza leo Jumatano Februari 19, 2020 Muliro  amesema Lulyeho alifariki wakati polisi wakimpeleka hospitali ya Wilaya kwa matibabu. Amesema tukio hilo lilitokea Februari 16, 2020 saa 10 jioni.

“Siku hiyo polisi walipokea taarifa kwamba shamba hilo limevamiwa na wahalifu waliokuwa wakiwashambulia  wafanyakazi wa shamba hilo waliokuwa katika hali mbaya karibu kupoteza maisha.”

“Walipofika walikuta wafanyakazi wawili wakiwa wamejeruhiwa vibaya. Polisi walipofika nao walianza kushambuliwa kwa mawe na askari wetu wawili walijeruhiwa,” amesema.

Amesema kundi la watu takribani  300 ilidaiwa waliingiza ng’ombe katika shamba hilo na kuanza kuwalisha kinyume na sheria, kanuni na utaratibu licha ya kupewa eneo la shamba hilo kulisha mifugo.

“Wafanyakazi hao walipowakataza ndio walianza kushambuliwa . Polisi walirusha mabomu ya machozi kuhakikisha wanatawanyika licha ya kuonywa watawanyike kabla ya mabomu. Walikaidi na kuanza kurusha mawe.”

Hali ilivyokuwa mbaya na wafanyakazi wanataka kuuawa, na mabomu kushindwa kuwatuliza,  risasi tatu zilipigwa hewani na moja ikawa imemjeruhi mmoja,” amesema.

Amesema baada ya mtu huyo  kujeruhiwa wenzake walimchukua, baadaye polisi walifuatilia na kubaini kuwa alipelekwa katika zahanati moja iliyopo eneo hilo.

“Polisi walimchukua kwa ajili ya kumpeleka hospitali ya wilaya lakini alifia njiani,” amesema Muliro.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?