Mapato ya ATCL yafikia Sh104.4bn

Mapato ya Shirika la Ndege ya Tanzania (ATCL) yameongezeka kutoka Sh24.7 bilioni mwaka 2016/17 hadi Sh104.4 bilioni mwaka 2018/19.

Dodoma. Mapato ya Shirika la Ndege ya Tanzania (ATCL) yameongezeka kutoka Sh24.7 bilioni mwaka 2016/17 hadi Sh104.4 bilioni mwaka 2018/19.

Kauli hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Moshi Kakoso juzi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo.

Pia, Kakoso alisema idadi ya abiria imeongezeka kwa wastani wa abiria 4,000 kwa mwezi mwaka 2015/16 hadi 45,000 mwaka 2018/19.

Alisema uwekezaji mkubwa wa Serikali umesababisha kupanuka kwa mtandao wa kutoa huduma.

Kakoso alisema hivi sasa ATCL inatoa huduma ya usafiri wa anga vituo 17 kati ya hivyo, 10 ni vya ndani ya nchi.

Alitaja vituo hivyo kuwa ni Bukoba, Dodoma, Dar es Salaam, Iringa, Kigoma, Kilimanjaro, Tabora, Mbeya, Mwanza na Zanzibar.

Vituo saba ni vya nje ya nchi Bujumbura Burundi, Entebbe Uganda, Hahaya Comoro, Harare Zimbabwe, Johannesburg Afrika Kusini, Lusaka Zambia na Mumbai India.

Hata hivyo, Kakoso alisema ATCL inakabiliwa na changamoto za uchache wa wataalamu hususan marubani na wahandisi washauri.

Alisema changamoto nyingine ni madeni yaliyolimbikizwa miaka ya nyuma yanayofikia Sh180 bilioni na kwamba, mwaka wa fedha 2019/20 ATCL ilitengewa Sh35.8 bilioni.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa taa za kuongozea ndege katika baadhi ya viwanja vya ndege jambo linalosababisha ndege kutua wakati wa mchana tu.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?