Kabendera awashukuru waandishi wa habari, aanza kuomboleza kifo cha mama yake

Dar es Salaam. Mwandishi wa Habari nchini Tanzania, Erick Kabendera amesema kwa sasa ndiyo anaanza maombolezo rasmi ya msiba wa mama yake mzazi, Verdiana Mujwahuzi.

Mama wa Kabendera, Verdiana  alifariki dunia Desemba 31, 2019, katika hospitali ya Amana Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kabendera amesema hayo, leo Jumatatu Februari 24, 2020 katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, muda mfupi baada ya kuachiwa huru na mahakama hiyo.

Baada ya kifo hicho, Kabendera aliwasilisha maombi mahakamani hapo akiomba aruhusiwe kwenda kuaga mwili wa mama yake katika shughuli ya mazishi iliyofanyika kanisa la Katoliki Temeke Dar es Salaam lakini hakuruhusiwa kwa madai Mahakama hiyo haikuwa na uwezo wa kusikiliza maombi yake.

Katika maelezo yake leo Jumatatu baada ya kuachiwa, Kabendera amewashukuru watu wa makundi mbalimbali kwa kumpigania katika kipindi chote wa kesi yake iliyodumu kwa zaidi ya miezi saba mahakamani hapo.

Ndugu wanataaluma wenzangu nawashukuru, waandishi wa habari, kunipigania kwa kipindi cha miezi saba nikiwa ndani, binafsi naomba niwashukuru waandishi wa habari kwa kunipa faraja na mmenitia moyo kusimama nami katika hali niliyokuwa nayo.”

Mmeniletea vitabu vya kusoma, kuniletea magazeti kusoma na mmenitia moyo. Nawashukuru ndugu zangu wa karibu, marafiki zangu wa karibu,” amesema Kabendera

Mwandishi huyo ya habari, ameachiwa huru na Mahakamani hiyo baada ya kukiri mashtaka mawili ambayo ni kukwepa kodi na kutakatisha fedha kiasi cha Sh173 milioni.

Hata hivyo, baada ya kukiri mashtaka hayo, mahakama  hiyo ilimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Sh250,000 au kwenda jela miezi mitatu, kwa kosa la kukwepa kodi.

Pia, katika shtaka la kukwepa kodi, Mahakama hiyo imehukumu mshtakiwa huyo, kuilipa Serikali fidia ya Sh172 milioni.

Katika fidia hiyo, mshtakiwa huyo ametakiwa kuilipa ndani ya miezi sita kuanzia siku iliposomwa Hukumu hiyo.

Katika shtaka la kutakatisha fedha kiasi cha Sh173 milioni mahakama imemuamuru kulipa faini ya Sh100 milioni baada ya kulipa faini.

Mshtakiwa huyo amefanikiwa kulipa faini zote na kubakisha fidia ya Sh172 milioni ambayo atailipa ndani ya miezi sita kuanzia siku hukumu iliyotolewa.

Kabla ya kutwa hatiani, mshtakiwa huyo alikuwa anakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha fedha kiasi cha Sh173 milioni.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) alimuondolea shtaka moja ambalo ni la kuongeza genge la uhalifu na hivyo kubaki na mashtaka mawili.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?