Unyonge wa Liverpool kwa miaka 30 EPL umefikia kikomo
Japo wenyewe hawasemi, ama yawezekana hawataki kunukuliwa wakisema, miaka 30 ya kushindwa kuchukua taji la Ligi ya Primia kwa Liverpool hatimaye inaelekea kufika kikomo. Hawawezi kusema hadharani, ama kuonesha furaha yao kwa sasa, kwa kuwa katika miaka hiyo 30 kumekuwa na vipindi ambavyo walikaribia kunyakua kombe lakini likawaponyoka. Lakini yaonekana mwaka huu hadithi ni tofauti, ubora wa kikosi ni wa hali ya juu, yawezekana ikawa sahihi kusema kikosi hiki cha sasa ndiyo bora zaidi kuliko vyote katika miongo mitatu iliyopita. Nuru ya ushindi iling'ara zaidi kwa vijana hao wanaonolewa na Mjerumani Jurgen Klopp baada ya kuichapa Leicester City inayoshika nafasi ya pili kwa goli 4-0 siku ya Boxing Day. Ushindi wa Liverpool uliambatana na kiwango safi cha umiliki wa kandanda, Leicester ambayo watu walikuwa wakiipigia chapuo la kuizuia Liverpool na kufanya maajabu ya kuchukua ubingwa kama mwaka 2016 walikuwa zaidi ya wanyonge katika mchezo huo uliopigwa dimbani kwao. Klopp:...