Uchaguzi wa Tanzania 2020: Bernard Membe ajiunga rasmi ACT-Wazalendo

Ni rasmi sasa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Bernard Membe amejiunga na chama cha upinzani ACT- Wazalendo
Uanachama wake mpya katika ACT- Wazalendo umetangazwa leo na kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe katika mkutano wa wanahabari wadau wengine kutoka ulimwenguni kote uliofanyika katika mtandao wa Zoom.
Membe amesema amejiunga kama mwanachama wa kawaida lakini yuko tayari kutumikia chama hicho kwa ngazi na namna yoyote ile.
"Kilichonivutia katika chama cha ACT-Wazalendo ni katiba ya chama hicho na itikadi yake ya kutaka kuleta mabadiliko," amesema Membe
Aidha bwana Zitto Kabwe amemtia moyo Membe kuchukua fomu kuwania nafasi ya uongozi.
Membe aliitikia kwa kuahidi kwamba atakuwa tayari kushiriki katika kinyang'anyiro cha uchaguzi.
"Watanzania watafurahia uchaguzi huu ujao," ameahidi Membe.
Kuhusu vyama vya upinzani kuungana na kuweka mgombea urais mmoja, Kabwe alisema mazungomzo baina ya vyama bado yanaendelea
Awali Kabwe alielezea mazingira ya uchaguzi ujao kuwa hayatapelekea uchaguzi ulio huru na wa haki akitaja pamoja na mambo mengine kutoamini uhuru wa tume ya uchaguzi na weredi wa jeshi la polisi
Newsday Swahili ilipomuuliza kwanini bado wataendelea na uchuguzi ilihali hawaamini mazingira kupelekea uchaguzi huru na wa haki Kabwe alisema kutokushiriki pia uchaguzi si jawabu la changamoto kwa demokrasia Tanzania.
"Tumeona katika uchaguzi uliopita visiwani Zanzibar na mahali pengine duniani ambapo vyama vya upinzani vilisusia uchaguzi lakini hakuna mabadiliko yoyote yaliyotokea. Hivyo kususia uchaguzi si jawabu" alisema Kabwe
Tanzania inaelekea katika uchaguzi mkuu mnamo mwezi Oktoba mwaka huu. Tayari chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekwisha teuwa wagombea wake wa urais kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Julai 6, mwaka huu bwana Membe alirejesha kadi ya uanachama wa Chama cha CCM.
Kiongozi huyo wa zamani alirudisha kadi ya uanachama ingawa Chama cha Mapinduzi kilishamfukuza uanachama .
Membe alidai kuwa taratibu za kichama hazikufuatwa, na hivyo bado alikuwa mwanachama halali wa CCM.

Tuhuma dhidi ya Membe ndani ya CCM

Membe alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kukiuka maadili pamoja na viongozi wengine waandamizi wengine wawili makatibu wakuu wa zamani Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, ambao wao hawajafukuzwa.
Katibu Mwenezi wa CCM Humphrey Polepole alidai kuwa mwenendo wa Membe ulikuwa si wa kuridhisha toka mwaka 2014.
"Kamati Kuu imeazimia kwa kauli moja kwamba Bernard Membe afukuzwe uanachama wa CCM. Uamuzi huu umekuja baada ya kuwa taarifa zake ndani ya chama zinaonesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 ambako katika chama amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumsaidia kujirekebisha," alieleza Polepole.

Madai ya hujuma

Membe amekuwa pia akituhumiwa na baadhi ya wanchama wa chama hicho kuwa najipanga 'kumhujumu' Magufuli katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Membe amekuwa akihusishwa kwa muda mrefu na mipango ya kutaka kugombea tiketi ya urais kupitia CCM mwaka huu, hatua ambayo baadhi wanaitafsiri kama usaliti.
Japo katiba ya CCM inaruhusu hilo, imekuwa ni ada ya chama kumuachia rais aliye madarakani kupita bila kupingwa kwa awamu ya pili ya urais.
Wakati huo tukio hilo lilitafsiriwa kwamba kufukuzwa kwa Membe ni kutokana na kuhusishwa huko na mipango ya Urais.

Follow us on Facebook


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?