Wanafunzi milioni 10 huenda wasirudi shuleni baada ya corona

Janga la virusi vya corona limesababisha dharura ya elimu ambayo haikutarajiwa huku takriban watoto milioni 9.7 wakiwa wameathiriwa kufuatia shule kufungwa na wako katika hatari ya kuacha shule kabisa.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Jumatatu na shirika la kimataifa la kuwahudumia watoto la Save the Children.
Shirika la Save the Children lenye makao yake makuu nchini Uingereza limetaja ripoti iliyotolewa mwezi Aprili na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, iliyosema kwamba jumla ya watoto bilioni 1.6- ikiwa ni takriban asilimia 90 ya jumla ya wanafunzi ulimwenguni kote, walilazimika kukosa elimu baada ya shule na vyuo vikuu kufungwa kufuatia masharti yaliyowekwa ya kuepusha kusambaa kwa virusi vya corona.
Kwenye ripoti yao mpya iliyotolewa leo, shirika hilo limesema kwamba kwa mara ya kwanza katika historia, masomo ya kizazi kizima cha wanafunzi ulimwenguni kote yametatizwa.
Shirika hilo limesema kwamba huenda mdororo wa uchumi ukawalazimisha kati ya wanafunzi milioni 90 hadi milioni 117, kutumbukia kwenye umaskini, hali itakayowaathiri kurudi shuleni.
Huku wanafunzi wengi wakihitajika kufanya kazi na wasichana kulazimika kuolewa mapema ili kuzisaidia familia zao, hali hiyo huenda ikasababisha kati ya wanafunzi milioni milioni saba hadi milioni 9.7 kuacha shule kabisa.
Wakati huo huo, shirika hilo limeonya kwamba janga hilo linaweza kusababisha bajeti za elimu katika mataifa yenye mapato jumla ya chini au ya wastani kupungua kwa dola bilioni 77 ifikapo mwisho wa mwaka 2021.
Mkuu wa shirika hilo Inger Ashing amesema takriban watoto milioni 10 huenda wasirudi shuleni kabisa, na kuitaja hali hiyo kuwa dharura ambayo haikutarajiwa. Amezitaka serikali kuwekeza kwa dharura katika masomo.
"Badala yake, tuko katika hatari ya bajeti kupunguzwa kwa njia zisizolingana, na hiyo itasababisha hali ya sasa ya ukosefu wa usawa kupindukia kati ya matajiri na maskini, na kati ya wavulana na wasichana.” Amesema Ashing.
Shirika hilo limezihimiza serikali pamoja na wadhamini kuwekeza zaidi kwenye mpango mpya wa elimu ulimwenguni, kuwawezesha wanafunzi kurejea shuleni wakati hali itakuwa salama, na pia kuendelea kuwasaidia elimu wakiwa nyumbani hadi hali itakapoimarika.
"Tunajua kwamba watoto maskini, waliotengwa zaidi na ambao tayari walikuwa nyuma zaidi wameathiriwa na kupata hasa kubwa, kwa kuwa hawawezi kupata elimu wakiwa nyumbani mfano kwa njia ya video au intaneti, au aina yoyote ya elimu hata kwa nusu mwaka.” Amesema Ashing.
Shirika la Save the Children limezihimiza taasisi za mikopo, kuwaahirishia watu wenye mapato ya chini ulipaji madeni, hali wanayosema itawezesha dola bilioni 14 kutengewa mipango ya elimu.

Mustakabali wa watoto kukumbwa na athari za muda mrefu

Ashing ameongeza kwamba tatizo lililopo sasa la elimu likiruhusiwa kuendelea, basi mustakabali wa watoto utakumbwa na athari za muda mrefu.
Huku akirejelea lengo la Umoja wa Mataifa, Ashing amesema ahadi ambayo ulimwengu umeweka wa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora ifikapo mwaka 2030, itarudishwa nyuma kwa miaka mingi.
Ripoti hiyo imeorodhesha nchi 12 ambako wanafunzi wako katika hatari kubwa ya kurejea nyuma, nazo ni Niger, Mali, Chad, Liberia, Afghanistan, Guinea, Mauritania, Yemen, Nigeria, Pakistan, Senegal na Ivory Coast.
Shirika hilo limesema kwamba hata kabla ya janga la corona, takriban watoto milioni 258 wakiwemo waliokwisha baleghe, tayari walikuwa nje ya shule.



Follow us on Facebook



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?