Virusi vya corona: Trump asema suala la kuvaa barakoa ni uchaguzi binafsi wa mtu

Rais Donald Trump, ambaye siku zote amekuwa akipinga muongozo wa uvaaji barakoa uliotolewa na maafisa wa afya, amesema atavaa barakoa kama atakuwa ''katika mazingira ya watu yatakayomlazimu kufanya hivyo''.
Bwana Trump ambaye amekwepa kujitokeza mbele Umma akiwa amevaa barakoa, pia amekuwa akishikilia msimamo wake kuwa kufunika uso hakuhitaji kuwa suala la lazima katika kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.
Kauli yake aliyoitoa kwa Fox News imekuja siku moja baada ya kiongozi wa Republican kutoa wito kwa Bwana Trump kuvaa barakoa ili aoneshe mfano.
Majimbo kadhaa nchini Marekani yameshuhudia ongezeko la maambukizi na vifo siku za hivi karibuni.
Marekani sasa ina watu zaidi ya milioni 2.6 waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya corona na vifo zaidi ya 127,000.

Rais amesema nini?

Akizungumza na kituo cha habari cha Fox Business Network siku ya Jumatano, Bwana Trump alisema : ''Ninaunga mkono barakoa.''
Alipoulizwa kama atavaa barakoa, rais alisema: ''Kama nitakuwa kwenye mazingira ambayo yatalazimu kufanya hivyo.''
Aliongeza kuwa watu wameshawahi kumuona akiwa amevaa barakoa hapo kabla.
Bwana Trump alisema ''hatakuwa na tatizo '' kuvaa barakoa mbele Umma akisema ''na ni kama anapenda'' anavyoonekana akiwa amevaa barakoa.
Lakini Rais amerejea tena msimamo wake kuwa hafikirii kuwa kufunika uso linahitaji kuwa suala la lazima nchini Marekani, kwa kuwa kuna ''maeneo mengi nchini humo ambayo watu hukaa kwenye umbali mkubwa''.
''Kama watu wanahisi vizuri kuhusu suala hilo wavae.''
Bwana Trump aliulizwa pia kama anaamini bado kuwa virusi vya corona siku moja ''vitatoweka''.
''Ninaamini'' alisema .Ndio hakika, Wakati wa sherehe zijazo za uhuru tarehe 3 mwezi Julai, watu watakaohudhuria wanaomuunga mkono hawatalazimika kuvaa barakoa wala kulazimishwa kutochangamana.

Trump alisema nini kuhusu barakoa?

Kituo cha kudhibiti magonjwa (CDC) mwezi Aprili kilipowataka watu kuvaa barakoa au kujifunika na nguo wanapokuwa maeneo ya watu wengi ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi, Bwana Trump aliwaambia wanahabari kuwa hatafuata kanuni hiyo.
''Sidhani kama nitafanya hivyo,'' alisema wakati huo.
''Kuvaa barakoa ninapowasalimia marais, mawaziri, maikteta, wafalme na malkia- kwa kweli sioni nikivaa.''
Lakini Trump amesisitiza mara kwa mara kuwa kuchagua kufuata muongozo wa wataalamu wa afya kuhusu barakoa ni suala la uamuzi binafsi.
Mwezi uliopita, aliliambia jarida la Wall Street kuwa baadhi ya watu huvaa barakoa kama jambo la kiasiasa dhidi yake.
Mwezi Mei, alipotembelea kiwanda kimoja mjini Michigan, aliwaambia wanahabari kuwa alivua barakoa kabla ya kufika mbele ya kamera kwa sababu ''hakutaka waandishi waione''.
Ikulu ya Marekani imetetea uamuzi wa rais kwa kusema kuwa kila mtu anayekutana naye hupimwa mara kwa mara kadhalika Rais Trump.
Binti wa Trump na mshauri wake mkuu, Ivanka Trump, pia alionekana akivaa barakoa akiwa mbele ya Umma.
Katika kura ya maoni ya Ipsos ilibainika kuwa katika kipindi cha juma lililopita, 89% ya Wamarekani walivaa barakoa walipokuwa wanatoka nje ya nyumbazo-kukiwa na ongezeko la alama 20 kutoka katikati ya mwezi Aprili.
Wanasiasa wamesemaje?
Trump amekua akikosolewa na Democrats kwa kupuuza kanuni ya uvaaji barakoa na kulifanya jambo hilo kuwa la kisiasa.
Lakini hivi karibuni vyombo vya habari vya Republican na Conservative vimeunga mkono suala la uvaaji barakoa.
Wakiwemo Makamu wa rais Mike Pence, anayeongoza kikosi kazi cha kupambana na Covid-19, Kiongozi wa wabunge wa seneti wa Republican Mitch McConnell, Seneta Mitt Romney na mbunge mwanamama Liz Cheney.
Siku ya Jumanne, seneta wa Republican wa jimbo la Tennessee Lamar Alexander alisema ni bahati mbaya kuwa ''hatua hii nyepesi ya kuokoa maisha imegeuzwa kuwa sehemu ya mjadala wa kisiasa ikisema ''kama unamuunga mkono Trump, hautavaa barakoa, ikiwa humuungi mkono utavaa.''
Siku hiyo hiyo, Mkurugenzi wa utafiti wa magonjwa Dkt Anthony Fauci aliwaambia wabunge kuwa inawezekana idadi ya watu wanaoambukizwa itafikia 100,000 kwa siku, na si Wamarekani wengi wanaovaa barakoa au kufuata kanuni ya kutochangamana.
Ongezeko la maambukizi limesababisha majimbo kadhaa kuahirisha mpango wa kuruhusu shughuli za kiuchumi kuendelea.
Kanuni ya kuvaa barakoa katika maeneo ya Umma ni suala la lazima kwa majimbo karibu 20 nchini humo.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Watalii wa Ufaransa kukabiliana na hukumu ya wizi wa mchanga