Uchaguzi wa Tanzania 2020: Nini mustakabali wa upinzani baada ya 'kifo' cha UKAWA?

Imesalia miezi mitatu kufanyika uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na madiwani nchini Tanzania ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
Hekaheka za kisiasa zimepamba moto miongoni mwa wanasiasa, vyama vya upinzani na chama tawala CCM kuanza michakato ya kupata wawakilishi wao wa majimbo mbalimbali, huku hatima ya uliokuwa muungano wa vyama vya upinzani UKAWA (Umoja wa Katiba ya Wananchi) ikiwa haijulikani na kuonesha dalili zote 'ulishazikwa rasmi'.
Uthibitisho wa 'kuzikwa' UKAWA uliotikisa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 umeoneshwa bayana baada ya hatua ya uongozi wa chama cha ACT-Wazalendo kuandika barua kuomba ushirikiano mpya na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku vyama vingine vikikaribishwa ikiwa maana hakuna umoja wowote kwa sasa, na haina uhakika kama vyama hivyo vitakubaliana kabla ya uchaguzi mkuu.
Katibu Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa nia ya kukiondoa CCM madarakani iko pale pale, hivyo wanahitaji ushirikiano mpya. "Tumewaandikia CHADEMA kuonesha kupokea hatua yao kwa mikono miwili na kuonesha utayari wetu wa kushirikiana katika uchaguzi ili kuiondosha CCM madarakani na kwakomboa watanzania,"
Je, vyama hivi viwili vitaweza kuinua ari ya wafuasi na wanachama wao ambao wapo kwenye mtihani mzito juu ya nini mustakabali wa vyama vya upinzani ikiwa havimo kwenye nguzo iliyoundwa na ambayo iliwapatia maelfu ya wabunge na madiwani na kura za urais milioni 6 kupitia aliyekuwa mgombea wao Edward Lowassa?
Duru za kisasa zinasema mustakabali wa UKAWA umo kwenye hatari ya kudidimia, mojawapo ya sababu ikiwa ni kutojulikana matakwa ya watanzania katika siasa za upinzani, kudhoofika mshikamano miongoni mwa vyama, ambao walipata mafanikio makubwa ya kisiasa za upinzani tangu kurejeshwa siasa za vyama vingi mwaka 1992 licha ya changamoto za kimkakati na uendeshaji na 'nyundo' wanazokutana nazo kutoka mamlaka za utawala.
Aidha, wachambuzi mbalimbali wa siasa na utawala bora wamebainisha kuwa kukosekana juhudi za viongozi wa vyama vya upinzani kunusuru UKAWA, mazingira ya kisiasa waliyopitia tangu mwaka 2015, kubanwa na mfumo wa utawala ikiwemo viongozi wake kukabiliwa na kesi mbalimbali mahakamani, kukosa ajenda na mikakati ya pamoja, ni sababu 'zinazozika' umoja huo.

Kupaa na kutunguliwa muungano wa UKAWA

Mwaka 2014 wakati wa Bunge la Katiba vyama vya upinzani viliunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutokana kutoridhishwa na mwenendo wa uendeshaji wa Bunge Maalum la Katiba na mchakato mzima wa katiba mpya. Ukawa ilidumu hadi ulipofika mchakato wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 ambapo viongozi waliendelea na mshikamano wao hivyo kuamua kuteua mgombea mmoja wa urais kupeperusha bendera chini ya umoja huo pamoja na kugawana majimbo na Kata.
Umoja huo ulipitia misukosuko kadhaa ambapo Agosti 2015 Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alijiuzulu wadhifa wake na kujiweka pembeni na Ukawa kwa kile alichodai kuwa ni kusutwa nafsi kutokana na umoja huo kumteua aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kugombea urais chini ya mwamvuli huo. Jambo hilo lilileta mkanganyiko mkubwa ndani ya umoja huo hasa upande wa CUF ambayo iligawanyika mara mbili kati ya waliomuunga mkono Profesa Lipumba na wengine walikuwa upande wa aliyekuwa Katibu Mkuu, Maalim Seif ambaye aliendelea na msimamo wa kumuunga mkono mgombea wa UKAWA.

Je, ni 'umoja' mpya nje ya UKAWA?

Taarifa za ACT-Wazalendo kutaka muungano wa kisiasa na CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu kumeibua mjadala zaidi huku baadhi ya wanazuoni wakiita nia hiyo ni sawa na kuanzisha umoja mpya wa UKAWA, lakini inaibua mashaka juu ya mustakabali wake kutokana na mwenendo wa NCCR-Mageuzi ambacho kimeibua msisimko mpya baada ya makada kadhaa wa CHADEMA kuhamia huko.
Dk. Richard Mbunda, ni mhadhiri wa Sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, amemwambia nwandishi kuwa, "Awali ya yote hatuwezi kutabiri kwa uhakika NCCR Mageuzi kuwa wanaweza kuleta matokeo kwa muungano huu wa CHADEMA na ACT-Wazalendo. Kuna uwezekano wa kuzigawa kura za upinzani. Nionavyo bila NCCR-Mageuzi na CUF muungano huu unaweza usipate nguvu kama ule wa UKAWA 2015,"
Hata hivyo, Ado Shaibu akisisitiza kuwa ni lazima wafanikishe mpango huo ili kutimiza azma yao ya kushika dola huku akiwaomba watanzania kuibua vuguvugu jipya la kisiasa.
Alipoulizwa swali kuhusu mustakabali wa UKAWA, alisema, "Ushirikiano ni matakwa ya Watanzania. Kila mmoja ameguswa na utawala wa usiofuata sheria wa Rais Magufuli, wafanyakazi wameguswa; wafanyabiashara wameguswa; wakulima wameguswa.
Orodha ni ndefu. Kinachosubiriwa ni msukumo wa kisiasa wa kuyaunganisha makundi yote haya ambao utaletwa na muunganiko wa kisiasa. Ni matumaini yangu kuwa hatua hii ya sasa tutakayochukua italeta vuguvugu jipya la kisiasa.,"

Vikwazo gani vinadhoofisha wapinzani?

Mhadhiri mmoja kutoka Chuo Kikuu nchini Scotland amemwambia mwandishi wa makala haya, "Vizingiti vya kimfumo vinavyowekwa haviwezi kuuruhusu upinzani wa aina yoyote kuwa na makali au kustawi kwa muda mrefu. Nawasifu sana wapinzani kuweza kuwa na matumaini na kuendelea kuthubutu.
Kimsingi kuanzia Tume ya Uchaguzi, Polisi, uongozi wa serikali za mitaa na mwelekeo mzima wa propaganda za kampeni, sioni kabisa nafasi ya wapinzani kupata haki zao hata wakiwa na sera na mikakati imara.
Huu mustakabali wao ni kitendawili, uchaguzi ni kama vile washindi wamekwisha amuliwa kabla hata ya kuanza. Bila kuwepo Tume huru ya uchaguzi, wapinzani wanapiga risasi gizani."

Je, ni upi mustakabali wa muungano wa UKAWA?


Frank Banka, mtaalamu wa masuala ya sayansi ya siasa na utawala bora, amemwambia mwandishi wa makala haya, "Mwaka 2015 makali ya muungano wa UKAWA yalitokana na mvuto wa wagombea wawili wakuu; John Magufuli (CCM) na Edward Lowassa (CHADEMA).
Kupitia mvuto huo ulichochea ongezeko la wanasiasa wapya wa vyama vya upinzani ambao hawakuwa hata na majina makubwa kwenye siasa wakati wa awamu ya nne chini ya Rais Kikwete.
Hii ndiyo maana ya watu kumshiba mwanasiasa badala ya itikadi za vyama husika, ambavyo kimsingi vina itikadi tofauti kabisa.
Kwa mfano mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (alipokuwa CUF), mbunge wa Kilombero Peter Lijualikali (CHADEMA) ni wanasiasa ambao hawakuwa na maarufu katika uwanja wa siasa nyakati za Kikwete,"
Ameongeza kwa kusema, "Mustakabali wao bado hauoneshi matumaini kwa mazingira ya sasa. Ile nguvu ya mwaka 2015 haionekani sasa.
Vyama hivi vinaweza kusimamisha mgombea mmoja kwenye nafasi ya urais kama watakubaliana upande wa Visiwani wabakie ACT-Wazalendo na Muungano waende CHADEMA. Hilo linaweza kuwasaidia. ACT wanamtegemea Zitto Kabwe upande wa Bara, na Maalim Seif upande wa Visiwani.
CHADEMA upande wa Bara wanaye Tundu Lissu lakini hawana nguvu Visiwani. Mustakabali wao utakuja pale vyama vya upinzani vitakapokuwa tayari, kuunganisha nguvu zao endelevu sio kwaajili ya uchaguzi wa mwaka 2020 peke yake, siasa ni vita endelevu."


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?