Jinsi rais Magufuli anavyopambana na corona na "mafisadi"

Rais wa Tanzania John Magufuli amekuwa akikosolewa kwa mashambulizi yake ya mara kwa mara dhidi ya "mabeberu" na tangazo lake la hivi karibuni kuwa maombi na sala vineondosha virusi vya corona katika taifa hilo.
Lakini suala hilo la kukosolewa huenda lisimsumbue kwa kuwa katika kipindi chake chore cha miaka mitano ya urais, amekuwa akijipambanua kama mzalendo wa kiafrika na mcha Mungu ambaye yupo kwenye mapambano dhidi ya mataifa ya magharibi ambayo yanataka kupora rasilimali za taifa hilo la Afrika Mashariki.
"Nataka watanzania mjue kuwa mna rais jiwe kweli. Siwezi tishwa na sitishiki," bwana Magufuli alisema Machi 2018.
Magufuli ana matumaini kuwa kazi yake inajieleza na itamsaidia kushinda uchaguzi ujao mwezi Oktoba na kurejea madarakani kwa muhula wa pili.
Moja ya mpambano mkubwa wa rais Magufuli ilikuwa dhidi ya kampuni kubwa ya madini ya Barrick Gold Corp ya nchini Canada.
Alitaka serikali ichukue udhibiti wa 60% katika migodi mitatu ya kampuni hiyo ili kukomesha "unyonywaji" wa rasilimali za Tanzania.
Magufuli mwenye miaka 60 sasa alianzisha majadiliano na Barrick ambayo yalionekana kama mzozo wa ng'ombe na sungura, na ijapokuwa serikali yake ilikubali kuchukua 16% ya hisa, mazungumzo hayo yalitosha kupeleka ujumbe kuwa mambo hayakuwa kama zamani nchini humo.
Akataa mradi wa 'mwendawazimu' na China
Baada ya kuingiwa makubaliano mapya baina ya Barrick na serikali mwezi Januari bosi wa kampuni hiyo Mark Bristow alisema mbele ya rais Magufuli kuwa: " Kilichofanyika hapa ni changamoto kwa sekta ya madini na kwetu sote kuanza safari ambayo tutapata pamoja ama kukosa pamoja."
Akiongea katika hafla hiyo, rais Magufuli hakuonesha tu upande wake wa kizalendo bali ucha Mungu, na kusema: " Namshukuru Mungu kwa mafanikio ya makubaliano haya."
Rais Magufuli pia amesitisha miradi miwili mikubwa baina ya nchi yake na China: ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme ya kati na ujenzi wa bandari kubwa ziadi Afrika Mashariki katika eneo la Bagamoyo kwa gharama za dola bilioni 10.
Magufuli alisema ni "mwendawazimu" tu ndiye angekubali masharti ya mradi huo ambayo yaliingiwa na serikali ya mtangulizi wake Jakaya Kikwete ili kujenga bandari hiyo.
Magufuli pia amekuwa akilaumu ubinafsi wa viongozi na kushindwa kutanguliza maslahi ya taifa kama chanzo cha nchi hiyo kutopiga hatua kubwa kimaendeleo.
Lakini ni mataifa ya magharibi ambayo rais Magufuli amekuwa akiyatilia mashaka zaidi, na amekuwa akiwatuhumu "vibaraka" wa mataifa hayo ndani ya nchi yake - ambao ni mchanganyiko wa wanasiasa wa upinzani, watetezi wa haki za binadamu na waandishi wakosoaji - kwa kupigania maslahi ya "mabeberu".
Mashaka yake na uzalendo umeenda mbali na kupelekea woga, mchambuzi kutoka Tanzania Thabit Jacob ameieleza Newsday Swahili.
"Anaminya upinzani, uhuru wa kijamii na harakati, vyombo vya habari na kufuatilia zaidi watu."

Hakuna safari za Magharibi

Mr Magufuli amerejesha tena matumizi ya neno "beberu" ambalo lilitumika sana nchini humo wakati wa kupigania uhuru na miaka ya awali baada ya uhuru kumaanisha nchi za magharibi.
Magufuli hajazuru hata nchi moja ya magharibi toka aingie madarakani. Kiongozi huyo pia hajahudhuria hata mkutano mkuu mmoja wa Umoja wa Mataifa (UNGA). Mikutano ya UNGA hutumiwa na viongozi wengine kutoka Afrika kama jukwaa la kueleza maoni na mipango yao kwa dunia.
Amehudhuria mikutano kadhaa ya Umoja wa Afrika (AU) na kutembelea nchi chache za Afrika ikiwemo Rwanda na Uganda, ambazo zinaongozwa na marais ambao hawafichi mashaka yao na nchi za magharibi.
Hata hivyo, anatanguliza maslahi ya nchi yake zaidi ya uzalendo wake kwa bara zima. Hakushiriki mikutano ya kikanda kuhusu janga la corona ambalo lilisababisha kufungwa kw a muda kwa mpaka wa Tanzania na Zambia pamoja na mpaka wa Tanzania na Kenya.
Tofauti na Uganda na Rwanda, Magufuli hakuweka marufuku ya watu kutoka nje kama njia ya kupambana na corona, akisema kuwa ingeongeza makali ya umasikini.

Je ni Tanzania pekee ndio haikufanga uchumi?

Kutoweka marufuku hiyo maarufu kama lockdown kulikariribisha ukosoaji mkubwa kutoka vyama vikubwa vya upinzani, ambavyo vilipendekeza kuwa miji yenye wakaazi wengi hususani Dar es Salaam ingefaa kuwekewa marufuku hiyo.
Hata hivyo, Magufuli si kiongozi pekee Afrika kuchukua hatua kama hizo.
Takwimu zilizokusanywa na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kupambana na Magonjwa (Africa CDC) zinaonesha kuwa takriban robo ya nchi za Afrika, ikiwemo Ethiopia, hazikufunga uchumi wake kupambana na corona.
Na mara baada ya mgonjwa wa kwanza wa corona kuthibitishwa nchini humu katikati ya mwezi Machi, Tanzania ilichukua hatua kadhaa za kuzuia maambukizi kama kufunga shule na michezo.
Hata kabla ya ugonjwa huo kutangazwa rasmi kuingia Tanzania Magufuli alipigwa picha maarufu ikimuoneha akisalimiana kwa miguu Ikulu jijini Dar es Salaam na kiongozi wa upinzani Maalim Seif Sharif Hamad baada ya wataalamu wa afya kutahadharisha juu ya salamu ya kupeana mikono.
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika bi Matshidiso Moeti aliikosoa Tanzania kwa kujivuta katika kupambana na maambukizi.
"Nchini Tanzania kwa hakika tumeona kuwa watu kuaacha kuchangamana, pamoja na kupiga marufuku kwa mikusanyiko ya watu wengi kumechukua muda mrefu kufanyika na tunaamini kuwa hayo yanaweza kuwa ni moja ya mambo yaliyopelekea ongezeko la kasi la wagonjwa wa corona," ameeleza Dkt Moeti mwezi Aprili.
Kwa wakosoaji, moja ya makosa makubwa ya rais Magufuli ni kuhimiza shughuli za ibada kuendelea licha tahadhari kutoka kwa wataalamu kuwa mikusanyiko ya kidini ni hatari kueneza maambukizi kwa kasi.
"Corona ni shetani. Haiwezi ikaishi kwenye mwili wa Yesu," alisema Magufuli mwezi Machi.
Na alipo hutubia kanisani hivi karibuni alisema: " Ugonjwa wa corona umeondolewa na Mungu."
Akihutubia bunge kwa mara ya mwisho Jumanne, Magufuli amerejelea kauli yake ya Mungu kujibu maombi na sala za Watanzania, na kuruhusu shule na shughuli zote zilizofungwa kutokana na corona kurejea kama awali. Japo, alisisitiza kuwa watu waendelee kuchukua tahadhari.

'Hujuma'

Siku moja kabla ya rais kulihutubia Bunge Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangza kuwa Tanzania imesalia na wagonjwa 66, hizo zikiwa takwimu rasmi za kwanza kutolewa toka mwishoni mwa mwezi Aprili baada ya rais Magufuli kitilia shaka takwimu na vipimo.
Katika baadhi ya hotuba zake Magufuli ameelezea mapambano ya Tanzania dhidi ya ugonjwa huo kuwa ni "vita" na kueleza mashaka yake dhidi ya "mipango ya mataifa ya nje."
"…Kuna mambo ya ajabu yanafanyika nchi hii. Ama wahusika wa maabara wamenunuliwa na mabeberu, ama hawana utaalamu jambo ambalo si kweli kwa kuwa maabara hii imetumika sana katika magonjwa mengine," alieleza Magufuli wakati akitilia mashaka ufanisi wa vipimo vya corona nchini humo.
"Nimesisitiza mara nyingi sinkila kitu unachopewa kutoka nje ni kizuri. Inawezekana kuna watu wanatumiwa, ama vifaa vikatumiwa...lakini pia inaweza kiwa hujuma kwa sababu hii ni vita."

Magufuli ni 'chuma'

Magufuli pia amepigia chapuo dawa za asili, ikiwemo kujifukizia na kinywaji cha miti shamba kutoka Madagascar kama njia za kupambana na corona licha ya WHO kuonya dhidi ya njia zote hizo mbili.
Magufuli anaziona nchi za Afrika kama washirika, ama walau kuwa siyo 'mabeberu', na kwa hivyo, anaona bora kushirikiana nazo na kutafuta tiba mbadala kwao kuliko nchi nyengine," anaeleza mchambuzi wa siasa za Tanzania Dan Paget.
Wataalamu wengi wa afya wanaamini viongozi - akiwemo rais wa Liberia George Weah - wanawajengea wananchi matumaini ya uongo, lakini dawa za mitishamba ni sehemu ya maisha ya waafrika wengi.
Takwimu za WHO zinaonesha kuwa 80% ya waafrika huzitumia. Endapo mbinu za Magufuli zimefanya kazi na kueleweka itafahamika zaidi miezi ijayo.
Kwa sasa amefanikiwa kujenga ushawishi kwa wenye siasa za kizalendo na wahafidhina wa kidini hali inayomfanya kuwa mstari wa mbele kushinda urais kwa awamu ya pili mwezi Oktoba.
Wakati Kikwete akiondoka madarakani mwaka 2015, alisema: "Naondoka, lakini tumewaletea hiki chuma."
Ilikuwa ni taswira halisi ya aina ya utawala wa Magufuli, ambao unasifiwa na wafuasi wake na kuchukiwa na wakosoaji wake.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?