Uchaguzi Tanzania 2020: Dini zina mchango gani katika siasa za Tanzania?

Katika hotuba yake ya kuaga Watanzania wakati akistaafu maisha ya kisiasa takribani miongo minne iliyopita, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisimulia kisa kinachoeleza uhusiano baina ya dini na siasa za Tanzania.
Alisimulia kisa kilichotokea wakati Tanganyika (ambayo Muungano wake na Zanzibar ndiyo umeunda Tanzania), ikipigania Uhuru wake dhidi ya wakoloni Waingereza.
Mwalimu Nyerere, alikuwa amechukuliwa na wazee wa chama cha TANU ambao wengi wao walikuwa waumini wa dini ya Kiislamu. Wakampeleka Bagamoyo, Pwani kwa ajili ya kufanya ibada maalumu ya kumwondoa mkoloni.
Kukatisha hadithi hiyo, Nyerere alieleza namna yeye (Mkristo), alivyokubalika na kupokewa na Waislamu wa Dar es Salaam kiasi cha kukabidhiwa madaraka ya juu zaidi hapa nchini.
Mkasa huu wa Baba wa Taifa la Tanzania unaeleza pia kuhusu ukweli mwingine kuhusu taifa hili; kwamba ingawa kuna dini mbili kubwa, kuna dini ya tatu ambayo huwa haisemwi sana lakini ina nguvu sana - dini ya nyumbani.
Tanzania ina mtanziko ambao umezikumba nchi nyingi za Afrika. Ukiangalia nchi zilizoendelea, dini zao ni mwendelezo wa mila na desturi za watu wa nchi hizo.
Ukristo una uhusiano mkubwa na mila na desturi za watu wa Ulaya. Uislamu una uhusiano mkubwa na mila za watu wa Mashariki ya Kati. Dini ya Kihindu ina uhusiano mkubwa na mila za Wahindi na unaweza kusema hivyohivyo kwa dini kama Budha, Shinto na nyinginezo nyingi.
Tanzania, kama zilivyo nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, dini kubwa za Ukristo na Uislamu, hazijajengwa kwenye misingi ya mila na desturi za Waafrika. Matokeo yake ni kwamba katika shughuli za kidini na kisiasa, kuna mambo yasiyo ya Kikristo wala Kiislamu, ambayo huingizwa ndani yake.
Katika mkasa wa Mwalimu Nyerere na wazee wa TANU, Nyerere alishuhudia mnyama akifukiwa akiwa hai katika tambiko. Pasi na shaka yoyote, matambiko ni sehemu ya utamaduni wa Mwafrika.
Kwa hiyo, kwenye kuzungumzia ushawishi wa dini katika siasa za Tanzania, ni lazima kutambua kwamba kimsingi kuna dini tatu kubwa hapa nchini; Wakristo, Waislamu na wale wanaofuata asili yao.
Unaweza kukuta mtu ni Mkristo au Muislamu safi lakini akiwa na tatizo asiende kwa Mchungaji au Sheikh wake lakini akaenda kwa 'mtaalamu' kwa ajili ya matibabu au ushauri wa mambo yake.
Katika uzoefu wangu kama mwandishi wa habari wa habari kwa zaidi ya muongo mmoja na nusu, nimejifunza kwamba kuna mambo ambayo Watanzania wanapata shida kukubaliana nayo na sababu haziko kwenye misingi ya kidini bali ni kwenye mila na tamaduni zao kongwe.
Wakristo au Waislamu, wapi ni wengi?
Katika siasa za Tanzania, hili ni miongoni mwa maswali ambayo yamepigwa marufuku kujadiliwa. Katikati ya miaka ya 1960, Serikali ya Tanzania ilikataza watu kuhojiwa dini zao katika Sensa ya Taifa.
Matokeo yake ni kwamba hadi leo kumekuwapo na utata kuhusu ni dini ipi ambayo ina wafuasi wengi kuliko nyingine. Kwa Tanzania, ni vigumu pia kujua idadi kamili ya watu wanaounda kabila fulani kwa sababu hilo pia lilipigwa marufuku kuulizwa.
Maswali hayo yaliondolewa kwa lengo la kujenga Umoja wa Kitaifa. Lengo lilikuwa kuzuia watu wa dini au kabila fulani kutumia wingi wao katika kufanya maamuzi ya kisiasa nyakati za uchaguzi.
Utafiti wa mwisho kufanyika hapa nchini na kutoa takwimu kuhusu dini hapa nchini ulifanywa na taasisi ya Pew mwaka 2010 na kuonyesha kwamba Wakristo ni asilimia 60 ya Watanzania wote huku Waislamu wakiwa asilimia 36 na dini nyingine wakibaki na asilimia nne.
Utafiti huu ulipingwa na baadhi ya viongozi wa Kiislamu waliodai kuwa hiyo ilikuwa ni propaganda ya kuonyesha kwamba Wakristo ndiyo wengi hapa nchini.
Katika 'busara' ya Kitanzania, huwa inajulikana kuwa kuna idadi inayolingana baina ya Wakristo na Waislamu. Kama kuna kupishana, asilimia inatakiwa kuwa ndogo lakini utafiti ule wa Pew ulileta utata kwa sababu ya kuonyesha pengo kubwa namna hiyo.
Ushawishi wa dini katika siasa za Tanzania
Katika historia ya takribani miaka 60 ya Tanzania, hakujawahi kuwa na uchaguzi ambao Watanzania walipiga kura zao kwa misingi ya dini zao. Msingi wa hili ulijengwa wakati wa harakati za kudai Uhuru.
Nyerere alikuwa Mkatoliki lakini karibu viongozi wengine wote wa juu wa TANU; wakiwamo wajumbe takribani 120 wa Baraza la Wazee walikuwa ni Waislamu. Kama Watanzania wangekuwa wanachagua kwa misingi ya dini, Nyerere asingepewa nafasi wala kuongoza taasisi hiyo.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Jakaya Kikwete alishinda kwa kupata asilimia zaidi ya 80 ya kura zote; ikimaanisha alipigiwa kura na watu wa dini zote.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015, wagombea wawili vinara; John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema walipata asilimia 60 na 40 ya kura zote zilizopigwa - ikimaanisha walipigiwa kura na wafuasi wa dini zote; ingawa wote walikuwa Wakristo.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu; haionekani kwamba dini itaamua nani awe mshindi. Wagombea wote wa Urais -Magufuli, Tundu Lissu wa Chadema na Bernard Membe wa ACT Wazalendo, wote ni Wakristo na kila mmoja anapendwa kwa sababu ya jambo tofauti lisilohusiana na dini zao.
Zanzibar na utofauti wake
Tofauti kubwa ya Zanzibar na Tanzania Bara ni kwamba walau visiwani inajulikana kwamba karibu watu wote ni waumini wa dini ya Kiislamu. Takwimu zinaonyesha walau asilimia 98 ya Wazanzibari ni Waislamu.
Kumekuwa na tuhuma za hapa na pale miongoni mwa washindani wa kisiasa wa visiwa hivyo kuhusu kutumia dini katika kutafuta kura; lakini ni vigumu sana kukwepa dini katika mazingira ambayo watu wote ni wa dini moja.
Kwa Zanzibar, ni vigumu kwa mgombea mwanamke kusimama jukwaani na kuomba kura akiwa hajajisitiri mwili wake kwa mujibu wa imani za Kiislamu kwa sababu inatarajiwa kuwa hivyo. Na huwezi pia kuomba kura kwa kuahidi vitu ambavyo dini ya Kiislamu inavikataza. Huwezi kupata kura.
Dini za kigeni na Dini ya nyumbani
Kwa ujumla, katika siasa za Tanzania, mengi ya mambo ambayo yanaweza kuhusishwa na dini katika mataifa ya Magharibi na Asia, kwa Tanzania dini ina ushawishi mdogo kuliko mila na desturi za Waafrika.
Kwa mfano, linapokuja suala la kukataa au kukubali ushoga na ndoa za jinsia moja; tatizo kubwa liko kwa wahafidhina wa mila na desturi kuliko hata dini. Ni watu wachache, kuondoa viongozi wa dini, wanaweza kutoa vifungu vinavyokataza mambo hayo kutoka katika vitabu vya dini, lakini wengi hukataza kwa sababu za maadili ya Kiafrika.
Wakati viongozi wa serikali wanapokataza mabinti wasirejee shuleni wakati wana mimba; tatizo huwa haliko kwenye dini lakini ni kwenye kucheza na akili za wahafidhina wa mila na desturi za Kiafrika - Kitanzania.
Katika suala nyeti kama umri wa watoto wa kike kuolewa; nyingi ya serikali za Afrika zimeamua kuacha watu wafuate dini na mila zao zinavyosema; badala ya kubana watu kwa sheria inayokata katikati.
Dini na siasa za sasa
Katika miaka ya karibuni, dunia inapita katika kipindi ambacho wanasiasa mufilisi wanatumia dini zao, rangi zao na makabila yao kuendesha siasa za kibaguzi.
Tanzania haijasalimika na vuguvugu hilo linaloendelea duniani kwa ujumla. Bahati nzuri pekee ambayo taifa hili inayo ni kwamba bado misingi yake ya umoja iliyowekwa wakati wa Uhuru haijatikiswa.
Wengi wa Watanzania hawako tayari kuchagua viongozi ambao waziwazi wanabagua watu wa dini, kabila au rangi nyingine. Mwanasiasa wa kawaida wa Tanzania huwa anahubiri kuhusu umoja pasipo kujali tofauti baina ya watu.
Kwa Tanzania, siasa ni kusingizia watu wa vyama vingine kuwa wana udini na wanatakiwa kuepukwa. Chama au mwanasiasa anayetaka kushinda uchaguzi kwa Tanzania, ni lazima aonyeshe kuwa anazitambua dini zote.
Ndiyo sababu, si ajabu kuona viongozi wote wa juu wa vyama vya Tanzania wakiwa wanaongozana na viongozi wa dini kwenye mikutano yao ya hadhara na wakifungua mikutano yao kwa maombi.
Kinachotakiwa ni kuhakikishia umma kwamba dini zote zitaruhusiwa kuendelea na shughuli zao na hakuna ambaye atabaguliwa au kutwezwa kwa sababu ya dini yake.
Na kama kiongozi atataka kufanyiwa dua au tambiko -kama Nyerere alivyofanyiwa na akina Sheikh Mohamed Ramia takribani miaka 60 iliyopita, basi ajue wapi pa kuwafuata na kuwapata.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?