Ni kwanini baadhi ya Wanyarwanda wanabadili majina yao?

Miaka 26 baada ya mauaji ya kimbari, Wanyarwanda wengi wenye majina yanayohusiana na makabila, majina yanayotaja kifo, maadui au dhana zingine wamechangamkia kubadilisha majina hayo na kuchukua majina mengine yenye maana chanya zaidi.
Jina ni utambulisho wa kila mtu na huambatana na maisha yake yote. Lakini nchini Rwanda, majina hubadilika kulingana na hali tofauti wanazopata wazazi na wakati mwingine siasa za nchi hiyo, na linaweza pia na maana ya ujumbe fulani kwa jamii.
Mwandishi wa BBC Yves Bucyana alitembelea katika maeneo tofauti ya Rwanda kuzungumza na wakazi ambao wamelazimika kubali majina ambao walimuelezea ni kwanini waliamua kufanya hivyo.
''Nina umri wa miaka 60 ,majina yangu ya kuzaliwa ni Gahutu Emmanuel lakini mwaka 1996 niliamua kubadili jina hilo kwa sababu linanihusisha na kabila na sikupenda kwendelea kuhusishwa na kabila kwani wakati huu Rwanda hakuna tena mambo ya ukabila. Nilipoomba kubadilisha serikali walinikubalia'', anasema Gahutu ambaye kwa sasa anatambulika kama Havugimana Emmanuel.
Jina lake jipya ''Havugimana" linamaanisha ''Mungu ndiye asemaye''.

Si Havugimana pekee aliyeamua kubadili jina lake

Nyirandizanye mkazi wa mji wa Gicumbi kaskazini mashariki, alikutana na Yves Bucyana alipokuwa akitoka kuwasilisha maombi ya kubadilisha jina:
''Wazazi waliniambia kwamba jina hilo lilitokana na kwamba mama alirudi nchini kutoka ukimbizini DRC akiwa na mimba kabla ya kunizaa alipofika Rwanda. Nilipokuwa mwanafunzi darasani kila mtu alikuwa anashangaa na kutaka kujua maana ya jina langu, likawa linanitia aibu ndiyo maana nataka libadilishwe na kuitwa Umuhoza -yaani mfariji ndilo jina linalonipa amani'', alisema.
Mtaalamu wa lugha nchini Rwanda Uwiringiyimana Jean Claude anasema Wanyarwana huwapatia majina watoto wao kwa sababu zao mbalimbali:
''Majina yote ya kinyarwanda yametiwa motisha...wazazi hutoa majina kwa watoto wao wakihamasishwa na hotuba na mazungumzo ya kijamii, imani,wengine wanatiwa motisha na hali za kibinafsi za familia, au pengine matukio yaliyopo nchini. Kabla ya mauaji ya kimbari utakuta kwamba watu walikuwa na majina yenye uhusiano na ukabila. Lakini kwa sasa ni majina ya yanayoepukwa.Kuna mambo mengi ambayo hayazungumziwi tena kwasababu sasa ni marufuku''
Kutokana na idadi kubwa ya watu wanaobadilisha majina wakati huu, wizara ya mambo ya ndani ilirahisisha taratibu za shughuli hiyo.
Chantal Mukayiranga afisa anayehusika na maswala hayo katika wizara ya mambo ya ndani anasema:
'' Mara nyingi haya ni majina yanayokera kidogo. Awali wengine waliniambia kuwa waliacha shule kwa sababu kila wakati walichekwa au kupigiwa kelele na wenzao. Halafu, maono ya wananchi wa Rwanda ya leo , hatutaki kuona mambo katika mwelekeo mbaya. Tunataka kuona mambo kwa mtazamo chanya, kwa umoja, hatuhitaji vitu vinavyoturejesha nyuma katika historia za uovu na uonevu''
Kulingana Bi Kayiranga, watu wengi kwa sasa wanapendelea majina kama Amahoro (amani), Ineza(fadhili) au hata Mutabazi (mwokozi), na mengineyo.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?