Macron akamilisha ziara Lebanon na onyo kwa viongozi

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewapa wanasiasa wa Lebanon hadi mwisho mwa mwezi Oktoba kuanza kutekeleza mageuzi, akisema msaada wa kifedha utazuiwa na baadaye kuwekewa vikwazo kama rushwa itazuia mchakato huo
Macron ameuambia mkutano wa wanahabari mjini Beirut kuwa viongozi wa kisiasa wamekubali kuunda serikali ya wataalamu katika wiki mbili zijazo kusaidia kuliweka kwenye mkondo sahihi taifa hilo la Mashariki ya Kati linalozidiwa na uzito wa mporomoko wa kiuchumi.
Macron amesema Paris iko tayari kusaidia kuandaa na kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa na Umoja wa Mataifa mwezi Oktoba. Rais huyo wa Ufaransa amesema vikwazo huenda vikatangazwa kama kutakuwa na ushahidi wa rushwa na vitaratibiwa na Umoja wa Ulaya, lakini hiyo sio mada ya Oktoba kwa sababu kwa sasa wapo katika mchakato wa kuaminiana na kushirikiana. "Nilisema hiki wazi, kama ikifika Oktoba, na walichokiahidi viongozi wenu hakijafanyika, tutahitaji kufanya maamuzi. Hii inamaanisha nini? inamaanisha hakuna kilichofanyika, kwa hiyo nitahitaji kuifahamisha jamii ya kimataifa kuwa hatuwezi kutoa msaada wetu. Lakini pia nitahitaji kuwaeleza Walebanon kuwa tulikuwa tayari kusaidia lakini viongozi wenu wakaamua vinginevyo." Amesema Macron

Katikati ya mji mkuu Beirut, polisi ya kukabiliana na ghasia na magari ya ulinzi walifyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji nje ya bunge waliokasirishwa na wanasiasa.
Macron alitembelea eneo la bandari lililokumbwa na mlipuko uliowauwa karibu watu 190 na akasema anataka ahadi halali za mpango wa mageuzi, ambao unajumuisha ukaguzi wa mahesabu ya benki kuu, na utaratibu wa kufuatilia, ukiwemo uchaguzi wa bunge katika miezi sita hadi 12. Rais huyo wa Ufaransa amesema alijaribu kuwashawishi wanasia kuwa sheria ya uchaguzi hazipaswi kuwa utangulizi wa mageuzi kwa sababu itasitisha kila kitu.
Shinikizo kutoka kwa Macron, ambaye alisema ataitembelea tena nchi hiyo Desemba, tayari imevisukuma vyama vikuu vya kukubaliana kuhusu waziri mkuu mpya, Mustapha Adib, ambaye ametoa wito wa kuundwa haraka kwa serikali na kuahidi kuyatekeleza haraka mageuzi ili kufikia makubaliano na Shirika la Fedha la Kimataifa - IMF. Katika siku za nyuma, kuunda baraza la mawiri kulichukua miezi kadhaa.
Macron aliadhimisha karne moja ya uhuru wa Lebanon kwa kupanda mti aina ya mwerezi katika msitu mmoja nje ya Beirut.
Rais huyo wa Ufaransa anaelekea leo nchini Iraq, katika jitihada iliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa kuimarisha uhuru wa nchi hiyo. Macron amesema ziara yake inalenga kuanzisha mpango mpya katika ushirikiano na Umoja wa Mataifa akiongeza kuwa Iraq imeteseka sana.
Follow us on Facebook
Follow us on Instagram
Follow us on Twitter
Subscribe our YouTube channel


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Watalii wa Ufaransa kukabiliana na hukumu ya wizi wa mchanga