Wagonjwa wanne wanaoshukiwa kuwa na virusi ya Corona wachunguzwa Ethiopia

Watu wanne wanaoshukiwa kuwa na virusi hatari vya corona wametengwa na wanafanyiwa uchunguzi zaidi katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa.

Tangu Jumatano iliyopita abiria wote wanaowasili katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Bole kutoka China wamekuwa wakifanyiwa uchunguzi kubaini kama wanaambukizwa virusi hivyo.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Addis Ababa, Waziri wa Afya wa Ethiopia Dkt. Liya Tadesse, amesema kuwa wagonjwa wanne wanaoshukiwa kuwa na virusi hatari vya corona wametengwa na wanafanyiwa uchunguzi zaidi.

Wagonjwa wote ni raia wa Ethiopia na kwamba watatu kati yao ni wanafunzi kutoka chuo kikuu cha eneo la Wuhan nchini China, ambako ni chimbuko la mlipuko wa virusi hivyo.

Maafisa wa afya wa Ethiopia wanasema kuwa sampuli ya damu imetolewa kwa wagonjwa hao na inatarajiwa kupelekwa Afrika Kusini kwa uchunguzi zaidi.

Kufikia sasa shirika la ndege la Ethiopia limewafanyia uchunguzi zaidi ya abiria elfu 22.

Awali mtu mmoja anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona nchini Kenya alipelekwa hospitalini.

Mshukiwa huyo ambaye ni mwanafunzi amefikishwa hospitali kuu ya rufaa ya Kenyatta jijini Nairobi.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa mtu huyo aliwekwa karantini alipowasili katika uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Nairobi, msafiri huyo raia wa Kenya alikua akitokea katika jiji la Guangzhou China na aliruhusiwa na maafisa afya wa Uchina kusafiri.

Hata hivyo, baada ya kuwasili jijini Nairobi maafisa afya katika uwanja wa Kenyatta walimuweka katika uangalizi maalumu kabla ya kuhamishiwa hospitali.

Je kuna tahadhari liyotolewa Kenya?

Hapo jana Kenya iliitahadharisha raia wake kwenda mji wa Wuhan China, mpaka pale mlipuko wa virusi hivyo utakapodhibitiwa.

Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ilisema ilikuwa na mawasiliano na raia wake waliokwama katika mji wa Wuhan, mji ambao ni kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo, ambao uko kwenye uangalizi maalum.

''Ubalozi unafahamu kuwa kuna raia wa Kenya 85 mjini Wuhan ambao wamesajiliwa ubalozini hivyo unafuatilia kwa karibu hali hiyo,'' wizara ilieleza kwenye taarifa yake hapo jana.

Kwenye mtandao wa Twitter , wakitoa ujumbe wao wa #KenyansInWuhan, wakenya waliokwama mjini Wuhan walitoa wito kwa serikali yao iwaondoe kwenye mji huo.

''Ni masikitiko tu kwa nchi yetu. Wiki ya pili sasa kwenye mji huu na hakuna lolote linalofanyika,'' aliandika kwenye ukurasa wa Twitter Cornelius Mulili.

''Hali hapa ni mbaya. Ilichofanya serikali yetu ni kutia taarifa kwa vyombo vya habari pekee. Sitaki kueleza tunachokipitia hapa kimwili na kiakili,'' alieleza Rono Kipkorir.

Tahadhari ya kusafiri imekuja siku chache baada ya maafisa nchini Ivory Coast kubaini mgonjwa aliyekuwa na dalili zinazofanan na mtu mwenye virusi vya corona. Haijathibitishwa kama mgonjwa huyo ana virusi hivyo.

Kenya ina moja kati ya viwanja vilivyo na pilikapilika nyingi barani Afrika na imeongeza umakini katika uangalizi wake. Inawapima abiria wote kutoka China.

Hivi ni virusi gani?

Virusi vyenyewe ni vipya - ambavyo huathiri wanyama.

Virusi hivi vinasababisha matatizo ya kupumua.

Dalili zake zinasemekana kuwa homa, kikohozi kikavu kisha baada ya wiki moja, mwathirika anakuwa na matatizo ya kupumua na kuhitaji matibabu kwa haraka.

Virusi hivyo vipya vinafananishwa na vile vya Sars, ambavyo vilisababisha vifo vya mamia ya watu 2003.

Hadi kufikia sasa, bado hakuna tiba maalum au chanjo dhidi ya virusi hivi.

Na kufikia Jumamosi, nchini Uchina kulikuwa na visa 1975 vilivyothibitishwa vya ugonjwa huo huku visa 2,684 zaidi vikishukiwa kuwa ni virusi hivyo, kulingana na Tume ya Taifa ya Afya ya Uchina.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?