Je, serikali ya Dolnald Trump kuzuia raia wa Tanzania kuingia Marekani?

Nchi nne za Afrika ikiwemo Tanzania zinaweza kupigwa marufuku raia wake kuingia nchini Mare
kani, vyombo vya habari vinaripoti.

Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vimeripoti vyanzo vinavyodai kuiona orodha ya nchi hizo ambayo inaweza kuwekwa wazi na serikali ya nchi hiyo Jumatatu ijayo, Januari 27.

Nchi nyengine za Afrika kwa mujibu wa ripoti hizo ni Nigeria, Sudan na Eritrea.

Rais wa Marekani, Donald Trump akiwa Davos nchini Uswizi amelithibitishia gazeti la Wall Street Journal kuwa ana mpango wa kuongeza idadi ya nchi kwenye orodha ya zuio la kuingia Marekani, lakini aligoma kuzitaja nchi hizo.

Kwa mujibu wa gazeti la Politico, rasimu ya nchi hizo bado haijakuwa rasmi na inaweza kubadilishwa.

Magazeti hayo pia, likiwemo la New York Times yanaripoti kuwa bado kuna mabishano baina ya maafisa wa Ikulu ya White House juu ya kujumuishwa ama kutolewa kwa nchi moja au mbili kwenye orodha hiyo.

Nchi nyengine nje ya Afrika ambazo zinasadikiwa kuwemo kwenye rasimu hiyo ya orodha ni Belarus, Myanmar na Kyrgyzstan.

Zuio hilo halitarajiwi kuwa la moja kwa moja ama kuathiri kila mtu bali aina fulani ya viza ama vinaweza kuwalenga maafisa wa serikali.

Kwa nini Tanzania 'iwe kwenye orodha?'

Licha ya vyombo hivyo vya Marekani kuitaja Tanzania lakini vyote havijaeleza kwa nini taifa hilo la Afrika Mashariki limo kwenye rasimu ya orodha.

Hivyo, licha ya taarifa hiyo kutarajiwa kupokewa kwa mshutuko na Watanzania, lakini maswali yataulizwa juu ya sababu za kujumuishwa ama hata kuhusishwa na orodha.

Majibu ya uhakika yanatarajiwa kupatikana wiki ijayo pale orodha hiyo itakapochapishwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la kimataifa la Reuters, afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Trump amewadokeza kuwa nchi ambazo zimeshindwa kufuata masharti ya kiusalama ikiwemo taarifa za alama za vidole, kupashana taarifa juu ya mapambano ya ugaidi yapo katika hatari zaidi ya kukumbwa na zuio hilo.

Gazeti la Politico linaripoti kuwa Wizara za Mambo ya Nje na Usalama wa Ndani Marekani zimekataa kuongelea juu ya rasimu hiyo mpya ya orodha.

Trump na vikwazo vya kuingia Marekani

Mwaka 2017 Trump alisaini zuio la kwanza la aina hiyo kwa nchi za Iran, Iraq, Syria, Yemen, Libya, Somalia, Chad, Venezuela na Korea Kaskazini.

Zuio hilo lilipingwa vikali hususani kwa kuzilega zaidi nchi zenye Waislamu wengi.

Awali zuio hilo lilipingwa kwa amri ya mahakama kabla ya Makama ya Upeo ya Marekani kukubaliana na hoja za upande wa Trump mwaka 2018.

Kwa upande wa Venezuela vikwazo vinawalenga viongozi wa serikali ya rais Nicolas Maduro ambayo Marekani haiitambui.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?