Watu wengi wa Taiwan wanaona kisiwa chao kama taifa tofauti
China imefanya mazoezi makubwa ya kijeshi kuzunguka Taiwan kwa mara ya pili mwaka huu - siku chache baada ya Rais wa Taiwan William Lai kutoa hotuba yake ya kwanza ya Siku ya Kitaifa.
Msingi wa mzozo wa China na Taiwan, ni madai ya China kuwa Taiwan inayojitawala yenyewe ni sehemu yake.
Beijing inakiona kisiwa hicho kama jimbo lililojitenga na ambalo huko mbeleni litakuwa sehemu ya nchi yake, na haijaondoa matumizi ya nguvu kufanikisha hili.
Lakini WaTaiwani wengi wanajiona kuwa sehemu ya taifa tofauti - ingawa wengi wanapendelea Taiwan ibaki kama ilivyo sasa, haijatangaza uhuru kutoka kwa China wala haisemi ni sehemu ya China.
Historia ya China na Taiwan
Walowezi wa kwanza wa Taiwan wa kabila la Austronesian, wanaoaminika walitoka kusini mwa China ya sasa ndio wanaojuulikana kuwa wa kwanza kuingia Taiwan.
Rekodi za Wachina zinaonekana kutaja kisiwa hicho kwa mara ya kwanza mwaka 239 AD, wakati mfalme alipotuma kikosi cha wasafiri huko - jambo ambalo Beijing hulitumia kuunga mkono madai yake juu ya eneo hilo.
Baada ya kuwa koloni la Uholanzi kwa muda mfupi, Taiwan ikawa chini ya ukoo wa Qing wa China, kabla ya kuwa chini ya Tokyo baada ya Japan kushinda Vita vya Kwanza vya Sino-Japan.
Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, Japan ilijisalimisha na kuacha udhibiti wa maeneo ambayo ilikuwa imeyachukua kutoka China. Ndipo, Taiwan ikatambuliwa rasmi kuwa inatawaliwa na Jamhuri ya China (ROC), ambayo ilianza kutawala kwa idhini ya washirika wake, Marekani na Uingereza.
Lakini katika miaka michache iliyofuata kulizuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini China, na kikosi cha Chiang Kai-shek kilishindwa na jeshi la Kikomunisti la Mao Zedong.
Chiang, sehemu ya serikali yake ya Kuomintang (KMT) na wafuasi wao takribani watu milioni 1.5 - walikimbilia Taiwan mwaka 1949.
Chiang alianzisha udikteta uliotawala Taiwan hadi miaka ya 1980. Baada ya kifo chake, Taiwan ilianza mpito wa demokrasia na ilifanya uchaguzi wake wa kwanza mwaka 1996.
Kuna kutokubaliana kuhusu Taiwan. Ina katiba yake, viongozi waliochaguliwa kidemokrasia, na wanajeshi wapatao 300,000 katika vikosi vyake vya jeshi.
Serikali ya Chiang mwanzoni ilidai inawakilisha China nzima, na ilinuia kuikalia tena. Ilikichukua kiti cha China kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ilitambuliwa na mataifa mengi ya Magharibi kuwa serikali pekee ya China.
Lakini kufikia miaka ya 1970 baadhi ya nchi zilianza kubishana kwamba serikali ya Taipei haiwezi tena kuchukuliwa kuwa mwakilishi wa kweli wa watu wanaoishi China Bara.
1971, Umoja wa Mataifa ulibadilisha maamuzi ya kidiplomasia na kuitambua Beijing. Mara baada ya China kuanza kufungua uchumi wake mwaka 1978, Marekani ilitambua fursa za biashara na haja ya kuendeleza mahusiano. Ilianzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia na Beijing mnamo 1979.
Tangu wakati huo idadi ya nchi zinazoitambua serikali ya ROC imeshuka kwa kiasi kikubwa na hadi sasa kuna nchi 12 pekee zinazokitambua kisiwa hicho leo. China inatoa shinikizo kubwa la kidiplomasia kwa nchi nyingine kutoitambua Taiwan.
Uhusiano wa Taiwan na China ukoje?
Mahusiano yalianza kuboreka katika miaka ya 1980 huku Taiwan ikilegeza sheria za kutembelea na kuwekeza nchini China. Mwaka 1991, ROC ilitangaza kwamba vita na Jamhuri ya Watu wa China vimekwisha.
China ilipendekeza chaguo linaloitwa "nchi moja, mifumo miwili.” Katika mfumo huo China itaruhusu uhuru mkubwa kwa Taiwan ikiwa itakubali kuwa chini ya udhibiti wa Beijing.
Mfumo huu ulisaidia kuirejesha Hong Kong chini ya China mwaka 1997 na namna inavyotawaliwa hadi hivi sasa, na Beijing inaongeza ushawishi wake.
Taiwan ilikataa mpango huo, na Beijing ikasisitiza kuwa serikali ya Taiwan sio halali - lakini wawakilishi wasio rasmi kutoka China na Taiwan waliendelea na mazungumzo.
Mwaka 2000, Taiwan ilimchagua Chen Shui-bian kama rais, jambo ambalo liliikasirisha sana Beijing. Chen na chama chake, Democratic Progressive Party (DPP), kiliunga mkono waziwazi "uhuru" wa Taiwan.
Mwaka mmoja baada ya Chen kuchaguliwa tena mwaka 2004, China ilipitisha sheria ya kupinga kujitenga, na kutangaza haki ya China kutumia "njia zisizo za amani" dhidi ya Taiwan ikiwa itajaribu "kujitenga" kutoka China.
Chen baadaye alirithiwa na chama cha KMT, ambacho kinapendelea uhusiano wa karibu na PRC.
Maoni
Chapisha Maoni