Uchaguzi Tanzania 2020: Je, namna gani wapiga kura wanaweza kuepuka migogoro wakati wa kampeni?



 Matukio ya vurugu za kisiasa miongoni mwa wapiga kura wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa urais,ubunge na udiwani unaoendelea nchini Tanzania yameathiri mahusiano moja kwa moja kutokana na itikadi tofauti za vyama vya siasa licha ya Katiba ya nchi hiyo kusisitiza uhuru wa kila mwananchi katika kuchagua itikadi hizo pamwe na kudumisha misingi ya demokrasia na siasa za vyama vya vingi.

Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na matamko ya vitisho dhidi ya wafuasi na wanasiasa wa pande mbili tofauti, kujinyonga, kupigana kwa kutumia mapanga na silaha zingine za jadi hali ambayo inachochea uvunjaji wa sheria pamoja na kuibua taharuki miongoni mwa familia, ndugu, marafiki na taifa kwa ujumla.

Duru za kisiasa zimetafsiri hali hiyo ni kiwango duni cha uvumilivu wa kisiasa miongoni mwa wapigakura, na kusababisha baadhi ya wapiga kura kuchukua uamuzi wa kukatisha uhai wao kwa sababu ya kutokukubaliana na wengine ndani ya familia, pamoja na viongozi kushindwa kuwa na lugha za ushawishi wafuasi wao kwenye masuala mbalimbali.

Migogoro inayotokana na tofauti za kiitikadi ni dhahiri watu wengi wanashindwa kuelewa maana halisi ya demokrasia ambapo kila mtu ana haki ya kuamini na kuwa na msimamo wa kile anachokiamini bila kulazimishwa na mtu mwingine.

Hoja hii inasimamiwa pia na Katiba ya Tanzania Ibara ya 21(2) isemayo; "Kila raia anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu taifa."

Je ni matukio yapi hatarishi?

Mnamo Oktoba 3 kuliripotiwa katika vyombo vya habari tukio la kijana wa miaka 22 kujinyonga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kamishna Msaidizi Abdi Isango alithibitisha kutokea kifo hicho mkoani humo kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 1 katika Kata ya Nsemulwa, Manispaa ya Mpanda.

Ilielezwa kifo cha kijana huyo kilitokana na kutofautiana kauli na mama yake mzazi, kuhusu mabishano ya kisiasa. Kijana anaripotiwa kuwa alikuwa mwanachama wa Chadema, wakati mama yake ni mwanachama wa CCM.

Kamanda Isango alisema mabishano hayo yalisababisha mama huyo kumchapa makofi mtoto wake hali ambayo ilimlazimu kutoweka nyumbani kwao na kurejea usiku kisha kujinyonga. Msingi wa mabishano hayo ni kijana kujaribu kumshawishi mama yake ahame CCM na kwenda Chadema.

Kisiwani Pemba kumeripotiwa matukio ya wanachama wa CCM kushambuliwa kwa mapanga, baadhi ya matukio hayo yakiripotiwa kufanyika msikitini.

Oktoba 17 mwaka huu gazeti la kila siku la Mwananchi lililiripoti msafara wa mgombea wa urais wa chama cha ADC, Queen Sendiga ulivamiwa na kundi la vijana ambao waliaminika wa CCM mkoani Iringa.

Msafara huo ulitoka Soko Kuu kwenda Stendi ya zamani mkoani humo. Hali hiyo sit u ilichochea taharuki bali ni kama kutangaza mgogoro wa kisiasa baina ya wanachama wa vyama hivyo.

Oktoba 6 mwaka huu vyama vya CCM na ACT Wazalendo mkoani Geita vililazimika kulaani matukio ya vurugu zilizotokea kwenye kampeni baina ya wafuasi wa CCM na Chadema zilizosababisha baadhi yao kujeruhiwa vibaya kwa kurushiana mawe na marungu hali iliyosababisha Polisi kuwatawanya kwa kuwapiga mabomu ya machozi.

Hayo ni baadhi ya matukio ya namna tatu; yale yanayohusisha familia moja kwa moja, makada binafsi na makundi ya wafuasi ambao wanatumika kuleta vurugu dhidi ya mengine hali ambayo inachochea migogoro ndani ya jamii, hasa hasa upande wa pili utaamua kuchukua njia hiyo hiyo kulipiza kisasi hivyo kuzua tafrani zaidi.

Inawezekana familia moja kuwa tofauti kisiasa?

Katika siasa familia kuwa katika itikadi tofauti za kisiasa ni jambo la kawaida na ambalo linasherehesha misingi ya demokrasia na siasa za vyama vingi.

Mathalani mbunge wa zamani wa Kigoma kusini, David Kafulila ni mfano wa karibuni, ambapo alipokuwa mwanachama wa NCCR Mageuzi, mkewe Jeska Kishoa ni mwanachama wa Chadema.

Ikumbukwe Kafulila alifukuzwa uanachama wa Chadema, na baadaye alihamia NCCR Mageuzi kabla ya kwenda CCM aliko sasa.

Hawa ni mume na mke ambao wanaonesha namna inavyowezekana familia moja kuwa na itikadi tofauti za vyama vya siasa, ambapo Jeska Kishoa ni miongoni mwa wagombea ubunge kwa tiketi ya Chadema mwaka huu.

Hivyo basi, tukitumia mfano huo mmoja tunaona inawezekana kabisa familia moja kufuata itikadi tofauti za kisiasa na zikakosa nafasi ya kuathiri familia husika.

Je, nini husababisha vurugu za kisiasa?

Duru za kisiasa zinaonesha kuwa miaka ya karibuni hali imebadilika kwa viongozi wa kisiasa ambao wanatumia nafasi zao kuhamasisha na kuaminisha wafuasi wao kuwa mawazo mbadala au itikadi inayopishana na yako ni uhaini au usaliti na hivyo hilo linastahili adhabu ama walau kutengwa.

Wafuasi wa CCM,ACT Wazalendo,ADC,NRA,AAFP,DP,SAU, Chadema, CUF na vingine wameaminishwa kuwa lazima wasikilize wanachama wenzao kuliko makundi mengine.

Wao hudhani uhuru wa mwanachi ni ule uliopo kwenye vyama hivyo. Mara kadhaa yametokea matukio baadhi ya vyama vya siasa kugombania kuzika mwili wa marehemu au kususiana misiba na majanga kwa sababu hayawahusu wafuasi wa itikadi nyingine.

Hata kwa baadhi ya viongozi wakiwa majukwaani hutamka kuwa \"wasipochagua chama changu hamtapata maendeleo\" au \"hapa mlikuwa na mwakilishi wa chama fulani na hatukuleta maendeleo kwa kuwa sisi ndiyo tunaoamua ba tusipofanya hamna la kutufanya\". Hizi ni kauli ambayo inatoa picha halisi ya kwamba nguvu na mamlaka ya wanasiasa wa Tanzania kwa sasa haitolewi kwa wananchi bali ni wanasiasa hivyo kuathiri wapigakura moja kwa moja.

Richard Ngaya, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha SUA na mchambuzi wa siasa na utawala bora amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa, "Matamshi ya viongozi wa vyama vya siasa ni miongoni mwa nyenzo za kwanza kutumiwa kwa wafuasi wao linapofika suala la kukabiliana na washindani wao kisiasa hutumika kama ngao ama muongozo kwa vile wafuasi huaminishwa ndivyo siasa anavyotakiwa kuenenda, kwamba hakuna ulazima wa kushirikiana na watu ambao si wanachama wenzako.

Anaongeza kwa kusema, "Katika siasa za aina hii miaka hii mitano chini ya kile kinachoitwa CCM mpya, siasa zimevuka mipaka na utamaduni ambao umekuwepo kwa miaka kadhaa ndani ya familia na jamii zetu.

Ilikuwa kawaida ndugu na jamaa kushirikiana kwa mambo ya kijamii huku wakijua kila mmoja na mtazamo wake kwenye masuala ya kisiasa japo pia kulishakuwepo baadhi ya watu kwenye familia kwa kuzingatia taarifa za baadhi za wabunge wa viti maalumu ama wabunge wa kuchaguliwa ndoa kuyumba kwa sababu za kisiasa.

Lakini pia kulishakuwepo mifano mingi ya ndoa ambazo pamoja na utofauti wa kisiasa wanandoa na wanafamilia walikuwa wamoja siku zote walau kwa jamii kutosikia misuguano kisa itikadi zao za kisiasa kutofautiana.

"Mtaani kwa sasa ni kawaida kuona watu wakisusiana kusaidiana matukio kadhaa kiitikadi kwa kuwa mwenye shida ni mfuasi wa chama fulani cha siasa, mfano iwe CCM,Chadema, CUF na ACT Wazalendo, hawawezi kushirikiana kijamii, hali inayojenga ufa wa mahusiano na rahisi kuibua matukio tatanishi kama ya Omary na wengine waliopitia kadhia hizo.

Ni njia zipi zinafaa kuzuia vurugu za kisiasa?

Mosi, wanasiasa ambao kwa kiasi kikubwa wenye nafasi ya kuleta maridhiano kwenye jamii wanapaswa kujihangaisha sasa kuondokana na kauli za kutishia hasa upande ambao si wao ama kutishia jamii juu ya vita iwapo watamchagua upande usio wao.

Kasoro hii iko kwenye itikadi za vyama vyote vya siasa, hakuna anajenga jamii yenye maelewano badala yake inajengwa jamii yenye utengano.

Pili, wananchi kutambua kuwa ni haki ya kila mmoja kujiunga na chama chochote kilichosajiliwa na kufuata sheria za nchi. Ni suala la haki ya kila mtu si idhini ya mwingine asiyehusika. Kinyume cha hayo haitakuwa tofauti na udikteta wa kidemokrasia.

"Suala hili limeota mizizi Tanzania, kwa upande wa wanawake kama mtakuwa na mtazamo tofauti wa kisiasa au mmoja hamuungi mkono mwenzake kutakuwa na shida, naweza kusema asilimia kubwa ya wanawake wakiingia siasa huku waume zao wakiwa si wanasiasa ndoa ina hatari kubwa kuvunjika. Kuna familia hawazungumzi kabisa kisa tofauti za kisiasa, mfano baba mzazi wa Ben Saanane hazungumzi na mwenyekiti wa Chadema, kwani mara kadhaa amelalamika kuwa Freeman Mbowe hakuwahi kumtembelea tangu alipopotea kijana wake. Hapo tayari ni mgogoro na familia hizi zimeathirika\"\".

"Sasa, unajua siasa ni imani, mtu anapenda chama chake hapendi kusikia mabaya kuhusu chama chake. Njia ya kuondokana na hilo ni kuelimisha jamii kuvumilaiana kiitikadi si chokochoko, kuongeza elimu ya uraia kuhusu siasa na kwamba kuwa itikadi tofauti si dhambi wala makosa. Njia nyingine ni vyama vya upinzani kuwaelimisha vijana ambao wanaunga mkono upande wao juu ya sheria Makosa ya Mitandaoni, ambapo vijana wengi wamepitia changamoto kubwa kwani hawana ufahamu nayo, hivyo kuwa chanzo cha migogoro kati ya familia,makundi,wafuasi na vyama vyao mara baada ya kukamatwa na vyombo vya dola. Tuwaelimishe kila upande ili wadumishe demokrasia kwa kuandaa vipindi vya redio, Televisheni,sanaa na maonesho na viongozi wa vyama wachukue hatua si kutelekeza wafuasi wao ambao ni rasilimali na viongozi wajao." anasema Theresia Mushi, Mwalimu, mwanasiasa na mchambuzi wa utawala bora.

Follow us on Facebook

Follow us on Instagram

Follow us on Twitter


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?