Urusi yakaribia kudhibiti mji muhimu wa Ukraine

        

Oparesheni ya Kyiv kwenye mji wa Kursk yadhoofika

.

CHANZO CHA PICHA,REUTERS

Urusi imepiga hatua kubwa katika siku za hivi karibuni ambayo inatishia kuzidi mafanikio yaliyopatikana na Ukraine katika shambulio lake la mpakani kwenye eneo la Kursk.

Vikosi vya Urusi viko kilomita chache tu kutoka mji wa Pokrovsk wa Ukraine, ambao ni muhimu sana kwaajili ya usafirishaji unaotumiwa na jeshi la Ukraine.

Pokrovsk ni mji wenye kituo muhimu cha usafiri wa reli na barabara kuu, na ni sehemu muhimu ya usambazaji na uimarishaji kwa wanajeshi wa Ukraine waliopo mstari wa mbele kwa upande wa Mashariki.

Wakosoaji ndani ya Kyiv wanahofia kuwa jeshi la nchi hiyo limefanya makosa makubwa.

Hatua ya kutuma wanajeshi kuvamia Kursk badala ya kuimarisha mstari wa mbele wa upande wa Mashariki, kumeacha Pokrovsk na miji mingine muhimu ya Ukraine kuwa hatarini, wakosoaji wanasema.

Rais wa Urusi Vladimir Putin alianza rasmi uvamizi wa Ukraine mnamo Februari 2022.

Akiwa kwenye ziara ya kutembelea wanajeshi wa mstari wa mbele, mkuu wa majeshi ya Ukraine Jenerali Oleksandr Syrskyi alisema Urusi ilikuwa inatumia "kila kitu inachoweza kutumia ili kuendelea mbele" kwenye mashambulizi yao wanayoyafanya.

"Hali ni ngumu sana," Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema siku ya Jumatano.

"Ikiwa tutapoteza Pokrovsk," mtaalam wa kijeshi Mykhaylo Zhyrokhov alionya, "mstari wote wa mbele utaanguka."

Kwanini Pokrovsk ni mji muhimu?

.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Pokrovsk upo karibu na mji mwingine wa Myrnohrad. Kwa pamoja, miji hii yenye makaazi ilikuwa na zaidi ya watu 100,000 idadi kabla ya vita, ambao wengi wao sasa wamekimbia. Ni miji mikuu ya mwisho katika sehemu hiyo ya eneo la Donetsk ambayo imesalia chini ya udhibiti wa Ukraine.

Vita vya Pokrovsk kwa kweli ni muendelezo wa vita vya Avdiivka, ambavyo Ukraine ilishindwa mnamo mwezi Februari, baada ya miezi kadhaa ya mapigano makali.

Avdiivka, uliopo takriban kilomita 40 (maili 25) Kusini-Mashariki mwa Pokrovsk, ulionekana kama ngome ambayo ililinda makaazi na barabara katika upande wake wa Magharibi na kusaidia kuimarisha uwepo wa Ukraine kwenye mstari wa mbele wote.

Avdiivka Ilipoanguka, kilichosalia ni magofu tu. Ilikuwa hasara kubwa kwa Ukraine.

Ilimaanisha kuwa Urusi inaweza kuelekeza nguvu zake nyingi kwenye mji wa Pokrovsk na mji muhimu wa Chasiv Yar, ambao unasimamia baadhi ya miji muhimu huko Donetsk, ambayo bado iko chini ya udhibiti wa Ukraine. Katika siku ya Jumamosi mapigano makali katika eneo hilo ya siku ya Jumamosi, yalisababisha vifo vya watu watano.

Kwa wiki kadhaa sasa, uhamishaji mkubwa wa raia wa Ukraine kutoka Pokrovsk umekuwa ukiendelea, huku maelfu ya watu wakisemekana kuwa wameondoka tayari.

Jenerali Syrskyi alisema analifanyia kazi suala la "kuimarisha ulinzi wa wanajeshi wetu katika maeneo magumu zaidi ya mstari wa mbele, kuwapa kikosi cha jeshi kiasi cha kutosha cha silaha za moto, vifaa na njia zingine za kiufundi".

Jinsi maendeleo ya Urusi yalivyopata nguvu zaidi

Kwa muda mrefu Urusi imekuwa ikishikilia Pokrovsk kama moja ya malengo yake makuu. Kwa miezi kadhaa vikosi vyake vimekuwa vikisafiri polepole kuelekea huko.

Wataalamu wanaamini kuwa Moscow imetuma karibu theluthi moja ya Kundi lake la Jeshi la Kati, au takriban wanajeshi 30,000, kwenye eneo hilo - pamoja na hifadhi zake zilizo tayari kwa vita.

Wiki hii, ilidhibiti mji wa Ukraine wa Novohrodivka, kitendo ambacho kimewakasirisha baadhi ya watu nchini Ukraine, ambao waliona kuwa ulipaswa kulindwa vizuri.

"Mahandaki mbele ya Novohrodivka yalikuwa tupu. Hakukuwa na jeshi la Ukraine katika eneo hilo lililokuwa na wanajeshi 20,000,” Mbunge wa Ukraine Mariana Bezuhla aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Huku vikosi vyake vikiwa na wanajeshi kidogo, na kuzidi idadi, inaaminika kuwa wanajeshi wa Ukraine waliondoka Novohrodivka ili kuimarisha ulinzi wake wa Pokrovsk.

"Kuna uwezekano kuwa amri ya Ukraine ilidhoofisha ulinzi wa Novohrodivka na haukustahili hasara iliyotokea," ilisema Taasisi ya Utafiti wa Vita yenye makao yake makuu mjini Washington (ISW). Kwingineko, vikosi vya Urusi vimeanzisha mashambulizi katika mji wa Selidove, kusini mwa Novohrodivka, na maeneo mengine ya karibu na eneo la Donetsk.

Mashambulizi ya Urusi yamesaidiwa na mabadiliko ya mbinu, ambazo zinazidi kuakisi zile zilizotumiwa mapema katika vita hivi na kundi la mamluki la Wagner.

Vikosi vya Ukraine vimeripoti kukabiliwa na mashambulizi makali kutoka kwa wanajeshi wa ardhini wa Urusi, waliotumwa katika jaribio la kuvamia maeneo yao.

Baadhi wameziita mbinu hizi kama mashambulizi ya nyama ambayo huhusisha idadi kubwa ya wanajeshi kuvamia adui bila kinga ama ngao yoyote ya kuwalinda.

Mbinu hii ambayo ina gharama kubwa – imemaliza kabisa nguvu ya vikosi vya kijeshi vya Ukraine kwa kuvilazimisha kujilinda na mashambulizi ya mara kwa mara.

Magari ya kivita hutumiwa kwa uangalifu – na kutatiza kazi ya mizinga ya Ukraine na silaha nyingine, ambazo zina vitu kidogo vya kulenga kwenye uwanja wa vita.

Urusi pia imekuwa ikitumia mabomu ya kuteleza yenye nguvu sana, na kulazimisha Ukraine kutawanya vitengo vyake wakati mashambulizi ya makombora yanapoanza na wakati mwingine hata kuwaondoa wanajeshi wake kwenye mstari wa mbele.

Hali ya uvamizi wa Ukraine katika mji wa Kursk

.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Mji wa Kursk

Wakati huo huo, maendeleo ya mashambulizi ya kihistoria ya kuvuka mpaka ya Ukraine yamedhoofika sana ndani ya wiki iliyopita.

Sudzha – ni makaazi makubwa zaidi ambayo Ukraine inadhibiti ndani ya Urusi – na yana wakaazi karibu 5,000, ambao ni mara tatu chini ya ile ya Novohrodivka, makazi ambayo Urusi ilidhibiti mapema wiki hii.

Siku ya Jumanne, kamanda mkuu wa jeshi la Ukraine alisema kuwa vikosi vya Kyiv vinamiliki kilomita za mraba 1,294 (maili za mraba 500) ndani ya Kursk, pamoja na makaazi 100 - na vimewakamata wanajeshi 594 wa Urusi katika harakati hizo.

Takwimu hizi zinapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari, lakini bila shaka ni muhimu. Swali ni kama watahalalisha hasara inayoweza kutokea kwenye vikosi vya mstari wa mbele katika eneo la Mashariki mwa Ukraine.

"Moja ya malengo ya operesheni ya kuelekea mji wa Kursk yalikuwa kupotosha vikosi muhimu vya adui kutoka pande zingine, haswa kutoka mwelekeo wa Pokrovsk na Kurakhove," Jenerali Syrskyi alisema hayo siku ya Jumanne.

Lakini lengo hilo linaonekana kushindwa. Vikosi vya Urusi havijatumwa tena kutoka mstari wa mbele wa Pokrovsk.

Badala yake wameimarishwa kwa kuongeza askari wa ziada na kufanya safari yao ya kuendelea mbele kuwa ya kasi sana.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Watalii wa Ufaransa kukabiliana na hukumu ya wizi wa mchanga