Ushindi wa William Ruto nchini Kenya unafundisha nini Tanzania?

Baada ya kuwatumikia Wakenya kwa miaka kumi akiwa Naibu wa Rais, sasa Bwana William Ruto ni rais mteule ambaye Wakenya wamempa kazi kubwa zaidi ya kuwa rais kwa miaka mitano ijayo; iwapo mambo yataendelea kubaki kama yalivyo sasa.

Ruto wa muungano wa Kenya Kwanza amemshinda mwanasiasa mkongwe bwana Raila Odinga, wa Azimio la Umoja kwa kupata asilimia 50.49 dhidi ya asilimia 48.85 za kura halali. Ushindi huo umemfanya Ruto kuwa mrithi wa kiti cha urais kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta akingojea kuapishwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kupitia ukurasa wake wa Twitter amewapongeza wananchi wa Kenya kwa kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu. Pia, akaahidi kuwa Tanzania itaendeleza udugu na ushirikiano wa kihistoria wa mataifa hayo.

Changamoto za ujirani 

Kenya ni ileile, jirani wa Tanzania. Kwa sasa kinachokwenda kubadilika ni kiongozi tu atakayeliongoza taifa hilo la wakazi zaidi milioni 54 kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2021.

Wakati hayati Rais John Pombe Magufuli akiwa madarakani, Kenya iliingia katika mvutano na Tanzania, katika sintofahamu kubwa juu ya mifugo na vifaranga kwa nyakati tofauti. Mivutano iliotikisa pakubwa uhusiano wa majirani hawa.

Kwa hakika Rais Samia Suluhu Hassan sio kiongozi wa misimamo mikali, hili lina maana kwamba rais mteule, William Ruto atakuwa na kazi nyepesi zaidi kushughulikia mvutano wowote utakaojitokeza na Tanzania.

Na kwa upande wa Tanzania, ina muda wa kusubiri kuziona sera za rais mpya panapohusika ujirani wao. Uhusiano wa Kenya na Tanzania hauishii tu katika ujirani, bali utengamano wa kibiashara ambayo hunufaisha pande zote mbili yanafanya ujirani wa maelewano kuwa muhimu zaidi.

Majirani wengine

Kwa wakati fulani nchi za Afrika Mashariki zimekuwa zikivutana, kila moja ikionekana kujichagulia rafiki na adui yake pia. Hapo awali, kabla mambo kukaa sawa, Uganda ikivutana na Rwanda, sasa Rwanda inavutana na Jamhuri ya Congo na Burundi.

Katika kampeni za uchaguzi, si William Ruto wala Raila Odinga aliyehubiri lugha ya kuiondoa Kenya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa maana hiyo hakuna shaka Kenya itaendelea kuwa mwanachama wa jumuiya.

Kuna kazi kubwa mbili: Mosi, ni kutimiza zile ahadi alizowaahidi Wakenya wakati wa kampeni zake, na hiyo ndiyo kazi kubwa zaidi. Pili; ni kushirikiana na mataifa jirani kuimarisha ustawi wa jumuiya.

Nchi za Afrika Mashariki zinategemeana kwa kiwango kikubwa katika kufanya biashara. Na kwa sasa Kenya haina mvutano na nchi yoyote miongoni mwa wanachama. Rais mpya atakuwa na nafasi nzuri zaidi kuleta mtangamano miongoni mwa majirani wanaovutana, sambamba na kuendeleza gurudumu la kusaidia kutatua changamoto za kiusalama. 

Kuna la kujifunza?

Kuanzia mwanzo wa uchaguzi hadi dakika za mwisho kabla ya kutangazwa matokeo, kulikuwa na mambo mengi ya kujifunza. Ingawa somo la demokrasia ya Kenya liliingia doa baada ya mgawanyiko wa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Hilo linatia doa ingawa halitofuta moja kwa moja yale mazuri yaliyoonekana katika siku za awali za kuanza kwa uchaguzi; ikiwemo uwazi katika zoezi zima la upigaji kura na amani na utulivu uliokuwepo.

Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete aliongoza timu ya uangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki, alipopata wasaa wa kuzungumza na waandishi wa habari alieleza juu ya uwazi wa uhuru alioushuhudia.

“Mawakala wote wa vyama vya siasa waliruhusiwa kuwa na smatiphone, pamoja na kupewa fomu, waliruhusiwa kuipiga picha na kuituma kwenye vyama vyao, sina hakika nchi zote zinafanya hivyo.”

Taarifa ya Ubalozi wa Marekani nchini Kenya, imepongeza juhudi za tume huru ya uchaguzi na mipaka, vyombo vya usalama na taasisi zote zinazohusika na uchaguzi, kwa kuiandaa kwa amani na mpangilio thabiti kazi ya upigaji kura na kuzihesabu.

Chaguzi za ubunge na ugavana zimekwenda vyema, kutoka mwanzo hadi mwisho. Kuhusu matokeo ya urais, kuna jambo linalosubiriwa; nalo ni ikiwa upande wa Odinga utakwenda mahakamani kama alivyosema mwenyewe Agosti 16 alipotangaza kutoyatambua matokeo ya uchaguzi.

Raila Odinga na Martha Karua

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Hapa kuna somo muhimu kwa Tanzania, ambayo mfumo wa kuhoji matokeo ya urais katika mahakama haupo kabisa katika katiba yake. Matokeo yanayotangazwa na tume ya uchaguzi, hakuna mwenye uwezo wa kuyajadili au kupinga kisheria. Yakitoka ndiyo yametoka!

Kuna sakata la makamishna wanne wa IEBC waliojiondoa wakiongozwa na makamu mwenyekiti, Juliana Cherera. Walieleza kwa vyombo vya habari kwamba hawakuhusika na uamuzi wa matokeo ya mwisho. Bado kuna yanayosubiriwa kutoka kwao.

Wakati huo huo Martha Karua mgombea mwenza wa Raila Odinga, kupitia ukurasa wake wa Twitter saa chache baada ya kutangazwa matokeo ya urais, aliandika ujumbe mfupi, “haijaisha hadi iishe.”

Kauli ya Karua na ile ya makamishna waliojiondoa, zinatoa dalili huenda matokeo yaliyompa ushindi Ruto yakafikishwa mahakamani. Mahakama ya Juu nchini Kenya ina historia nzuri, katika kushughulika kesi za uchaguzi ikiwemo kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais mwaka 2017. 

Hadi sasa William Ruto ndiye rais mteule. Kuna wanaosubiri hatima ya matokeo ya urais wakiamini yatakwenda mahakama. Ila kwa hakika Kenya inazidi kupiga hatua katika demokrasia yake ya uchaguzi, licha ya changamoto zilizojitokeza.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Urusi kuisadia Uganda kujenga uwezo wake wa nyuklia, ni mataifa gani ya Afrika yanatumia nishati ya nyuklia na kwanini?