Marekani na Ulaya zaonya wanajeshi wa Eritrea kuingia Tigray


Marekani na Umoja wa Ulaya zimeelezea wasiwasi wao kuhusu kupelekwa hivi karibuni kwa majeshi ya Eritrea kwenye jimbo la Tigray nchini Ethiopia, ambako pameshuhudiwa vita vilivyodumu kwa miezi tisa.

Vikosi kutoka Tigray vilidhibiti tena eneo kubwa la jimbo hilo mwezi Juni, ikiwa ni pigo kubwa kwa serikali ya Ethiopia. Lakini kupelekwa tena kwa vikosi vya Eritrea, miezi kadhaa baada ya Ethiopia kusema majeshi ya kigeni yalikuwa yakiondoka, kunazusha hofu ya kuongezeka mapigano zaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema nchi yake ina wasiwasi kwamba idadi kubwa ya majeshi ya ulinzi ya Eritrea yameingia tena Ethiopia, baada ya kuondoka mwezi Juni. Blinken ameyatoa matamshi hayo wakati ambapo wizara ya fedha ya Marekani imetangaza vikwazo dhidi ya mkuu wa jeshi la Eritrea anayetuhumiwa kwa kukiuka haki za binaadamu wakati wa vita vya Tigray. Eritrea imesema madai hayo hayana msingi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken

Wakati huo huo, Agosti 20, mabalozi wa Umoja wa Ulaya waliandika taarifa ya ndani kwamba Eritrea ilikuwa inapeleka vikosi vyake katika jimbo la Tigray. Taarifa hiyo iliyoonekana na shirika la habari la Reuters imeeleza kuwa majeshi ya Eritrea yamepelekwa kwenye eneo la magharibi mwa Tigray na kujihami kwa vifaru na silaha za kivita kwenye miji ya Adi Goshu na Humera.

Abiy alizuru Asmara

Aidha, taarifa hiyo ilisema pia kwamba Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed aliuzuru mji mkuu wa Eritrea, Asmara Agosti 17, ziara ambayo haikutangazwa na ofisi yake, wakati akiwa njiani kuelekea kwenye mkutano wake rasmi nchini Uturuki. Hata hivyo wasemaji wa wizara ya habari ya Eritrea, ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia na jeshi la Ethiopia, hawajalizungumzia suala hilo.

MADA ZINAZOHUSIANA

Huku hayo yakijiri, Ethiopia imeanza kuwaandikisha wahitimu kwa ajili ya kupambana na waasi wa Tigray. Mateso yaliyowakumba raia hao, yamesababisha wananchi wa Ethiopia kuchukua silaha kupambana na waasi wa Tigray.

Seid Mohammed Hussein, msimamizi wa eneo la Wollo Kusini anasema kuwa wakiitikia wito uliotolewa na Waziri Mkuu Abiy kuhusu uhamasishaji, watu hao wamesema wako tayari kupambana.

Wakimbizi wa Tigray waliokimbia vita

\"\"Vikosi vya kigeni pia vinapambana dhidi yetu, ikiwemo Marekani na nchi nyingine za kigeni ambazo zinaunga mkono vita hivi kwa njia isiyofaa. Waethiopia wote wanalijua wazi hili,\"\" alifafanua Hussein.

Mwezi Aprili serikali ya Ethiopia ilisema majeshi ya Eritrea yameanza kuondoka Tigray, lakini msemaji wa vikosi vya Tigray amerudia kusema kuwa wanajeshi wa Eritrea bado wako jimboni humo.

Vita kati ya vikosi vya serikali ya shirikisho ya Ethiopia na Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF vilizuka mwaka uliopita na tangu wakati huo zaidi ya watu milioni mbili wamelazimika kuyakimbia makaazi yao. Majeshi ya Eritrea yaliingia Tigray kupambana sambamba na vikosi vya shirikisho, ambapo kulingana na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu mzozo huo umesababisha unyanyasaji ikiwemo ubakaji.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Umoja wa Ulaya hatimaye wakubaliana kuufufua uchumi wao

Watalii wa Ufaransa kukabiliana na hukumu ya wizi wa mchanga